| ← Job (38/42) → |
| 1. | Ndipo Bwana akamjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema, |
| 2. | Ni nani huyu atiaye mashauri giza Kwa maneno yasiyo na maarifa? |
| 3. | Basi jifunge viuno kama mwanamume, Maana nitakuuliza neno, nawe niambie. |
| 4. | Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya nchi? Haya! Sema, kama ukiwa na ufahamu. |
| 5. | Ni nani aliyeamrisha vipimo vyake, kama ukijua? Au ni nani aliyenyosha kamba juu yake? |
| 6. | Misingi yake ilikazwa juu ya kitu gani? Au ni nani aliyeliweka jiwe lake la pembeni, |
| 7. | Hapo nyota za asubuhi zilipoimba pamoja, Na wana wote wa Mungu walipopiga kelele kwa furaha? |
| 8. | Au ni nani aliyeifunga bahari kwa milango, Hapo ilipofurika kana kwamba imetoka tumboni. |
| 9. | Nilipolifanya wingu kuwa vazi lake, Na giza zito kuwa nguo ya kuifungia, |
| 10. | Nikaiagiza amri yangu; Nikaiwekea makomeo na milango, |
| 11. | Nikasema, Utafika mpaka hapa, lakini hutapita, Na hapa mawimbi yako yanyetayo yatazuiliwa? |
| 12. | Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza? Umeyajulisha mapambazuko mahali pake? |
| 13. | Yapate kuishika miisho ya nchi, Waovu wakung'utwe wakawe mbali nayo? |
| 14. | Hubadilika mfano wa udongo chini ya muhuri, Vitu vyote vinatokea kama mavazi. |
| 15. | Na waovu nuru yao huzuiliwa isiwafikie, Na mkono ulioinuka huvunjika. |
| 16. | Je! Umeziingia chemchemi za bahari, Au umetembea mahali pa siri pa vilindi? |
| 17. | Je! Umefunuliwa malango ya mauti, Au umeyaona malango ya kuzimu? |
| 18. | Umeyafahamu mapana ya dunia? Haya! Sema, ikiwa unayajua hayo yote. |
| 19. | Iko wapi njia ya kuyafikia makao ya nuru? Na giza pia, mahali pake ni wapi? |
| 20. | Upate kuipeleka hata mpaka wake, Upate kuelewa na mapito ya kuiendea nyumba yake? |
| 21. | Hukosi unajua, maana ulizaliwa wakati huo, Na hesabu ya siku zako ni kubwa! |
| 22. | Je! Umeziingia ghala za theluji, Au umeziona ghala za mvua ya mawe, |
| 23. | Nilizoziweka akiba kwa wakati wa misiba, Kwa siku ya mapigano na vita? |
| 24. | Je! Nuru hutengwa kwa njia gani, Au upepo wa mashariki hutawanywaje juu ya nchi? |
| 25. | Ni nani aliyepasua mfereji kwa maji ya gharika, Au njia kwa umeme wa radi; |
| 26. | Kunyesha mvua juu ya nchi isiyo na watu; Juu ya jangwa asiyokaa mwanadamu; |
| 27. | Kuishibisha nchi iliyo kame na ukiwa, Na kuyameza majani yaliyo mororo? |
| 28. | Je! Mvua ina baba? Au ni nani aliyeyazaa matone ya umande? |
| 29. | Barafu ilitoka katika tumbo la nani? Na sakitu ya mbinguni ni nani aliyeizaa? |
| 30. | Maji hugandamana kama jiwe, Na uso wa vilindi huganda kwa baridi. |
| 31. | Je! Waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia, Au kuvilegeza vifungo vya Orioni? |
| 32. | Je! Waweza kuziongoza Sayari kwa wakati wake? Au waweza kuongoza Dubu na watoto wake? |
| 33. | Je! Unazijua amri zilizoamuriwa mbingu? Waweza kuyathibitisha mamlaka yake juu ya dunia? |
| 34. | Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni, ili wingi wa maji ukufunikize? |
| 35. | Waweza kuutuma umeme, nao ukaenda, Ukakuambia, Sisi tupo hapa? |
| 36. | Je! Ni nani aliyetia hekima moyoni? Au ni nani aliyetia ufahamu rohoni? |
| 37. | Ni nani awezaye kuyahesabu mawingu kwa hekima? Au ni nani awezaye kuzimimina chupa za mbinguni? |
| 38. | Wakati mavumbi yagandamanapo, Na madongoa kushikamana pamoja? |
| 39. | Je! Utamwindia simba mke mawindo? Au utashibisha njaa ya simba wachanga, |
| 40. | Waoteapo mapangoni mwao, Wakaapo mafichoni wapate kuvizia? |
| 41. | Ni nani anayempatia kunguru chakula, Makinda yake wanapomlilia Mungu, Na kutanga-tanga kwa kutindikiwa na chakula? |
| ← Job (38/42) → |