| ← Job (34/42) → |
| 1. | Tena Elihu akajibu na kusema, |
| 2. | Sikilizeni maneno yangu, enyi wenye hekima; Tegeni masikio kwangu, ninyi mlio na maarifa. |
| 3. | Kwa kuwa sikio huyajaribu maneno, Kama vile kaakaa lionjavyo chakula. |
| 4. | Na tujichagulie yaliyo ya uelekevu; Na tujue wenyewe yaliyo mema. |
| 5. | Kwani Ayubu amesema, Mimi ni mwenye haki, Naye Mungu ameniondolea haki yangu; |
| 6. | Nijapokuwa mwenye haki, nimehesabiwa kuwa mwongo; Jeraha yangu haiponyeki, nijapokuwa sina makosa. |
| 7. | Je! Ni mtu gani mfano wa Ayubu, Anywaye mzaha kama maji? |
| 8. | Atembeaye na hao watendao uovu, Na kwenda pamoja na watu wabaya. |
| 9. | Kwa kuwa amenena, Haimfai mtu lo lote Kujifurahisha na Mungu. |
| 10. | Kwa hiyo nisikilizeni, enyi wenye fahamu; Mungu asidhaniwe kutenda udhalimu; Wala Mwenyezi kufanya uovu. |
| 11. | Kwani atamlipa binadamu kwa kazi yake, Naye atamfanya kila mtu kuona sawasawa na njia zake |
| 12. | Naam, hakika, Mungu hatatenda mabaya, Wala Mwenyezi hatapotosha hukumu. |
| 13. | Ni nani aliyemwagiza kuiangalia dunia? Au ni nani aliyemwekea ulimwengu huu wote? |
| 14. | Kama akimwekea mtu moyo wake, Akijikusanyia roho yake na pumzi zake; |
| 15. | Wenye mwili wote wataangamia pamoja, Nao wanadamu watarejea tena kuwa mavumbi. |
| 16. | Ikiwa una ufahamu, sikia neno hili; Isikilize sauti ya maneno yangu. |
| 17. | Je! Atatawala mtu aichukiaye haki hata mmoja? Nawe, je! Utamhukumia mkosa aliye na haki na mwenye nguvu? |
| 18. | Je! Inafaa kumwambia mfalme, Wewe u mwovu? Au kuwaambia wakuu, Ninyi ni wabaya? |
| 19. | Sembuse huyo asiyependelea nyuso za wakuu, Wala hawajali matajiri kuliko maskini? Kwani wote ni kazi ya mikono yake, |
| 20. | Hufa ghafula, hata usiku wa manane; Watu hutikisika na kwenda zao, Nao mashujaa huondolewa pasipo mkono wa mtu. |
| 21. | Kwani macho yake ya juu ya njia za mtu, Naye huiona miendo yake yote. |
| 22. | Hapana weusi, wala hilo giza tupu, Wawezapo kujificha watendao udhalimu. |
| 23. | Kwani yeye hana haja ya kumfikiria mtu zaidi, ili aende mbele za Mungu ahukumiwe. |
| 24. | Yeye huwavunja-vunja mashujaa pasina kuwachunguza, Na kuwaweka wengine mahali pao. |
| 25. | Kwa sababu hiyo yeye huyatafiti matendo yao; Naye huwapindia usiku, wakaangamia. |
| 26. | Yeye huwapiga kama watu wabaya Waziwazi mbele ya macho ya wengine; |
| 27. | Kwa sababu walikengeuka, wasimwandame yeye, Wasikubali kuzishika njia zake hata moja; |
| 28. | Hata wakafanya kilio cha maskini kumfikilia, Naye akasikia kilio cha hao wateswao. |
| 29. | Akitoa utulivu yeye, ni nani awezaye kuhukumia makosa? Akificha uso wake, ni nani awezaye kumtazama? Kama hufanyiwa taifa, au mtu mmoja, ni sawasawa; |
| 30. | Kwamba huyo mpotovu asitawale, Pasiwe na wa kuwatega watu. |
| 31. | Kwani kuna mtu aliyemwambia Mungu, Mimi nimevumilia kurudiwa, ingawa sikukosa; |
| 32. | Nisiyoyaona nifundishe wewe; Kama nimefanya uovu sitafanya tena? |
| 33. | Je! Malipo yake yatakuwa kama upendavyo wewe, hata ukayakataa? Kwani yakupasa wewe kuchagua, si mimi; Kwa sababu hiyo sema uyajuayo. |
| 34. | Watu walio na akili wataniambia, Naam, kila mtu mwenye hekima anisikiaye; |
| 35. | Huyo Ayubu amesema pasipo maarifa, Na maneno yake hayana hekima. |
| 36. | Laiti Ayubu angejaribiwa hata mwisho, Kwa kuwa amejibu kama watu waovu. |
| 37. | Kwani huongeza uasi juu ya dhambi zake, Apiga makofi kati yetu, Na kuongeza maneno yake kinyume cha Mungu. |
| ← Job (34/42) → |