| ← Job (32/42) → |
| 1. | Basi hao watu watatu wakaacha kumjibu Ayubu, kwa sababu alikuwa mwenye haki machoni pake mwenyewe. |
| 2. | Ndipo zikawaka hasira za huyo Elihu mwana wa Barakeli, Mbuzi, katika jamaa ya Ramu, juu ya Ayubu, kwa sababu alikuwa amejipa haki mwenyewe zaidi ya Mungu. |
| 3. | Tena hasira zake ziliwaka juu ya hao rafiki zake watatu kwa sababu hawakupata jawabu, lakini wamemhukumia Ayubu makosa. |
| 4. | Basi huyo Elihu alikuwa anangoja ili anene na Ayubu, kwa sababu hao wengine walikuwa wazee kuliko yeye. |
| 5. | Hata Elihu alipoona kuwa hapana jawabu katika vinywa vya watu hao watatu, hasira zake ziliwaka. |
| 6. | Basi Elihu mwana wa Barakeli, Mbuzi, akajibu, na kusema, Mimi ni kijana, na ninyi ni wazee sana; Kwa hiyo nilijizuia, nisithubutu kuwaonyesha nionavyo. |
| 7. | Nilisema, Yafaa siku ziseme, Na wingi wa miaka ufundishe hekima. |
| 8. | Lakini imo roho ndani ya mwanadamu, Na pumzi za Mwenyezi huwapa akili. |
| 9. | Sio wakuu walio wenye akili, Wala sio wazee watambuao hukumu. |
| 10. | Basi nilisema, Nisikilizeni mimi; Mimi nami nitawaonyesha nionavyo. |
| 11. | Tazama, niliyangojea maneno yenu, Nilizisikiliza nisikie hoja zenu, Hapo mlipokitafuta mtakalonena. |
| 12. | Naam, niliwasikiza ninyi, Na tazama, hapana mmoja aliyemshinda Ayubu, Wala kumjibu maneno yake, kati yenu. |
| 13. | Jitunzeni msiseme, Sisi tumepata hekima; Mungu yumkini akamshinda, si mtu; |
| 14. | Kwa kuwa yeye hajayaelekeza maneno yake kwangu; Wala sitamjibu mimi kwa maneno yenu. |
| 15. | Wameshangaa, hawajibu tena; Hawana neno la kusema. |
| 16. | Na mimi, je! Ningoje, kwa sababu hawaneni, Kwa sababu wasimama kimya, wala wasijibu tena; |
| 17. | Mimi nami nitajibu sehemu yangu, Mimi nami nitaonyesha nionavyo. |
| 18. | Kwa kuwa nimejaa maneno; Roho iliyo ndani yangu hunihimiza. |
| 19. | Tazama, tumbo langu ni kama divai iliyozibwa; Kama viriba vipya li karibu na kupasuka. |
| 20. | Nitanena, ili nipate kutulia; Nitafunua midomo yangu na kujibu. |
| 21. | Tafadhali, nisiupendelee uso wa mtu; Wala sitajipendekeza kwa mtu ye yote. |
| 22. | Kwani mimi sijui kujipendekeza; Au Muumba wangu angeniondoa kwa upesi. |
| ← Job (32/42) → |