| ← Job (3/42) → |
| 1. | Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na kuilaani siku yake. |
| 2. | Ayubu akajibu, na kusema; |
| 3. | Na ipotelee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, Na ule usiku uliosema, Mtoto mume ametungishwa mimba. |
| 4. | Siku hiyo na iwe giza; Mungu asiiangalie toka juu, Wala mwanga usiiangazie. |
| 5. | Ishikwe na giza, giza tupu, kuwa yake; Wingu na likae juu yake; Chote kiifanyacho siku kuwa giza na kiitishe. |
| 6. | Tena usiku huo, na ushikwe na giza kuu; Usihesabiwe katika siku za mwaka; Wala kutiwa katika hesabu ya miezi. |
| 7. | Tazama, usiku huo na uwe tasa; Wala isiwe ndani yake sauti ya shangwe. |
| 8. | Na waulaani hao waulaanio mchana, Hao walio tayari kumwamsha huyo lewiathani. |
| 9. | Nyota za mapambazuko yake na ziwe giza; Na utafute mwanga lakini usiupate; Wala usiyaone makope ya asubuhi; |
| 10. | Kwa sababu haukuifunga milango ya tumbo la mamangu. Wala kunifichia taabu machoni. |
| 11. | Mbona si kufa mimi tokea mimbani? Mbona nisitoe roho hapo nilipotoka tumboni? |
| 12. | Mbona hayo magoti kunipokea? Au hayo maziwa, hata nikanyonya? |
| 13. | Maana hapo ningelala na kutulia; Ningelala usingizi; na kupata kupumzika; |
| 14. | Pamoja na wafalme na washauri wa dunia, Hao waliojijengea maganjoni; |
| 15. | Au pamoja na wakuu wenye dhahabu, Waliozijaza fedha nyumba zao; |
| 16. | Au, kama kuzikwa mimba iliyoharibika, nisingekuwako; Kama wachanga wasiouona mwanga kabisa. |
| 17. | Huko waovu huacha kusumbua; Huko nako hao waliochoka wapumzika |
| 18. | Huko wafungwa waona raha pamoja; Hawaisikii sauti yake msimamizi. |
| 19. | Wakuu na wadogo wako huko; Mtumishi yu huru kwa bwana wake. |
| 20. | Mbona yeye aliye mashakani kupewa mwanga, Na hao wenye uchungu rohoni kupewa uhai; |
| 21. | Ambao wangojea mauti, lakini hawayapati; Na kuyachimbulia zaidi ya kutafuta hazina iliyostirika; |
| 22. | Ambao wafurahi mno, Na kushangilia watakapoliona kaburi? |
| 23. | Kwa nini mtu aliyezibiwa njia kupewa mwanga, Ambaye Mungu amemzingira kwa ukingo? |
| 24. | Kwani kuugua kwangu kwaja kana kwamba ni chakula, Na kunguruma kwangu kumemiminika kama maji. |
| 25. | Maana jambo hilo nichalo hunipata, Nalo linitialo hofu hunijilia. |
| 26. | Mimi sioni raha, wala situlii, wala kupumzika; Lakini huja taabu. |
| ← Job (3/42) → |