← Job (28/42) → |
1. | Hakika kuna shimo wachimbako fedha, Na mahali wapatapo dhahabu waisafishayo. |
2. | Chuma hufukuliwa katika ardhi, Na shaba huyeyushwa katika mawe. |
3. | Binadamu hukomesha giza; Huyatafuta-tafuta hata mpaka ulio mbali, Mawe ya giza kuu, giza tupu. |
4. | Hufukua shimo mbali na makao ya watu; Husahauliwa na nyayo zipitazo; Huning'inia mbali na watu, huyumba-yumba huko na huko. |
5. | Katika ardhi ndimo kitokeamo chakula; Na chini yake hupinduliwa kama kwa moto. |
6. | Mawe yake ni mahali zipatikanapo yakuti; Nayo ina mchanga wa dhahabu. |
7. | Njia ile hapana ndege mkali aijuaye, Wala jicho la tai halijaiona; |
8. | Wanyama wakali wajivunao hawajaikanyaga, Wala simba mkali hajaipita. |
9. | Huunyoshea mwamba wa gumegume mkono wake; Huipindua milima hata misingi yake. |
10. | Hukata mifereji kati ya majabali; Na jicho lake huona kila kito cha thamani |
11. | Hufunga vijito visichuruzike; Na kitu kilichostirika hukifunua. |
12. | Bali hekima itapatikana wapi? Na mahali pa ufahamu ni wapi? |
13. | Mwanadamu hajui thamani yake, Wala haionekani katika nchi ya walio hai. |
14. | Vilindi vyasema, Haimo ndani yangu; Na bahari yasema, Haiko kwangu. |
15. | Haipatikani kwa dhahabu, Wala fedha haitapimwa iwe thamani yake. |
16. | Haiwezi kutiwa thamani kwa dhahabu ya Ofiri, Wala kwa shohamu ya thamani nyingi, wala kwa yakuti ya samawi. |
17. | Dhahabu na vioo haviwezi kulinganishwa nayo; Wala kubadili kwake hakutakuwa kwa vyombo vya dhahabu safi. |
18. | Havitatajwa fedhaluka wala bilauri; Naam, kima cha hekima chapita marijani. |
19. | Yakuti ya rangi ya manjano ya Kushi haitasawazishwa nayo, Wala haitatiwa kima kwa dhahabu safi. |
20. | Basi hekima yatoka wapi? Na mahali pa ufahamu ni wapi? |
21. | Kwa kuwa imefichwa mbali na macho ya wote walio hai, Na kusitirika na ndege wa angani. |
22. | Uharibifu na Mauti husema, Tumesikia habari zake kwa masikio yetu. |
23. | Mungu ndiye aijuaye njia yake, Naye anajua mahali pake. |
24. | Maana anatazama hata miisho ya nchi, Na kuona chini ya mbingu nzima. |
25. | Apate kuufanyia upepo uzito wake; Naam, anayapima maji kwa kipimo. |
26. | Hapo alipoiwekea mvua amri, Na njia kwa umeme wa radi. |
27. | Ndipo alipoiona na kuitangaza; Aliithibitisha, naam, na kuichunguza. |
28. | Kisha akamwambia mwanadamu, Tazama, kumcha Bwana ndiyo hekima, Na kujitenga na uovu ndio ufahamu. |
← Job (28/42) → |