| ← Job (27/42) → |
| 1. | Kisha Ayubu akaendelea na mithali yake, na kusema, |
| 2. | Kama aishivyo Mungu, aliyeniondolea haki yangu; Huyo Mwenyezi aliyeitesa nafsi yangu; |
| 3. | (Kwa kuwa uhai wangu ukali mzima ndani yangu, Na roho ya Mungu i katika pua yangu;) |
| 4. | Hakika midomo yangu haitanena yasiyo haki, Wala ulimi wangu hautatamka udanganyifu. |
| 5. | Hasha! Nisiwahesabie ninyi kuwa na haki; Hata nitakapokufa sitajiondolea uelekevu wangu. |
| 6. | Haki yangu naishika sana, wala sitaiacha; Moyo wangu hautanisuta wakati nikiwapo hai. |
| 7. | Adui yangu na awe kama huyo mwovu, Na mwenye kuondoka kinyume changu na awe kama asiye haki. |
| 8. | Kwani tumaini la mpotovu ni nini, ingawa ajipatia faida, Hapo Mungu amwondoleapo roho yake? |
| 9. | Je! Mungu atakisikia kilio chake, Taabu zitakapomfikilia? |
| 10. | Je! Atajifurahisha katika Mwenyezi, Na kumlingana Mungu nyakati zote? |
| 11. | Nitawafundisha ninyi mambo ya mkono wa Mungu; Hayo yaliyo kwa Mwenyezi sitayaficha. |
| 12. | Tazama, ninyi nyote mmeyaona wenyewe; Mbona basi mmebatilika kabisa? |
| 13. | Hii ndiyo sehemu ya mtu mwovu kwa Mungu, Na urithi wa hao waoneao, waupokeao kwa Mwenyezi. |
| 14. | Watoto wake wakiongezeka ni kwa upanga; Na wazao wake hawatashiba chakula. |
| 15. | Hao watakaosalia kwake watazikwa katika kufa, Wala wajane wake waliofiwa na waume hawataomboleza. |
| 16. | Ajapokusanya fedha kama mavumbi, Na kujifanyia mavazi kama udongo kwa wingi; |
| 17. | Yumkini kuyatengeza, lakini wenye haki watayavaa, Nao wasio na hatia watazigawanya hizo fedha. |
| 18. | Yeye hujenga nyumba yake kama mdudu, Na kama kibanda afanyacho mlinzi. |
| 19. | Yeye hujilaza hali ni tajiri, lakini ndio mwisho; Hufunua macho yake, naye hayuko. |
| 20. | Vitisho vyampata kama maji mengi; Dhoruba humwiba usiku. |
| 21. | Upepo wa mashariki humchukua, naye huondoka; Na kumkumba atoke mahali pake. |
| 22. | Kwani Mungu atamtupia asimhurumie; Angependa kuukimbia mkono wake. |
| 23. | Watu watampigia makofi, Na kumzomea atoke mahali pake. |
| ← Job (27/42) → |