← Job (26/42) → |
1. | Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, |
2. | Jinsi ulivyomsaidia huyo asiye na uwezo! Jinsi ulivyouokoa mkono usio na nguvu! |
3. | Jinsi ulivyomshauri huyo asiye na hekima! Na kutangaza ujuzi wa kweli kwa wingi! |
4. | Je! Umetamka maneno kwa nani? Kisha ni roho ya nani iliyotoka kwako? |
5. | Hao waliokufa watetema Chini ya maji na hao wayakaao. |
6. | Kaburi li wazi mbele yake, Uharibifu nao hauna kifuniko. |
7. | Yeye hutandaza kaskazi juu ya nafasi isiyo na kitu, Na kuutundika ulimwengu pasipo kitu. |
8. | Huyafunga maji ndani ya mawingu yake mazito; Na hilo wingu halipasuki chini yake. |
9. | Husitiri uso wa kiti chake cha enzi, Na kulitandaza wingu lake juu yake. |
10. | Amepiga duara kuwa ni mpaka juu ya uso wa maji, Hata hapo mwanga na giza vinapopakana. |
11. | Nguzo za mbingu zatetemeka, Na kustaajabu kwa kukemea kwake. |
12. | Huichafua bahari kwa uwezo wake, Na kumtema Rahabu kwa akili zake. |
13. | Hizo mbingu hupambwa kwa roho yake; Mkono wake umemchoma nyoka aendaye mbio. |
14. | Tazama, hivi ni viunga tu vya njia zake; Na jinsi yalivyo madogo manong'ono tusikiayo katika habari zake! Lakini ngurumo za uweza wake ni nani awezaye kuelewa nazo? |
← Job (26/42) → |