Job (23/42)  

1. Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,
2. Hata leo mashitaka yangu yana uchungu; Pigo langu ni zito zaidi ya kuugua kwangu.
3. Laiti ningejua mahali niwezapo kumwona, Nifike hata hapo anapokaa!
4. Ningeiweka daawa yangu mbele yake, Na kukijaza kinywa changu hoja.
5. Ningeyajua maneno atakayonijibu, Na kuelewa na hayo atakayoniambia.
6. Je! Angeshindana nami kwa ukuu wa uwezo wake? La, lakini angenisikiliza.
7. Hapo walekevu wangepata kuhojiana naye; Basi hivyo ningeachiliwa na mwamuzi wangu milele.
8. Tazama, naenda mbele, wala hayuko; Narudi nyuma, lakini siwezi kumwona;
9. Na mkono wa kushoto, afanyapo kazi, lakini siwezi kumwona; Hujificha upande wa kuume, hata nisimwone.
10. Lakini yeye aijua njia niendeayo; Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.
11. Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake; Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka.
12. Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu,
13. Lakini yeye ni mmoja, ni nani awezaye kumgeuza? Tena nafsi yake ilitakalo, ndilo afanyalo.
14. Kwani yeye hulitimiliza hilo nililoamuriwa; Tena mambo mengi kama hayo ya pamoja naye.
15. Kwa hiyo naona taabu mbele ya uso wake; Nitakapofikiri, namwogopa.
16. Kwani Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia, Naye Mwenyezi amenitaabisha;
17. Maana sikufadhaishwa kwa sababu ya giza, Wala kwa sababu giza kuu limenifunika uso.

  Job (23/42)