| ← Job (22/42) → |
| 1. | Ndipo huyo Elifazi Mtemani akajibu, na kusema, |
| 2. | Je! Yumkini mtu awaye yote kumfaa Mungu? Hakika yeye aliye na hekima hujifaa mwenyewe. |
| 3. | Je! Mwenyezi hupata furaha katika wewe kuwa mwenye haki? Au je, ni faida kwake, kwamba wafanya njia zako kuwa timilifu? |
| 4. | Je! Ni kwa wewe kumcha yeye anakukemea? Na kuingia hukumuni nawe? |
| 5. | Je! Uovu wako si mkuu? Wala maovu yako hayana mwisho. |
| 6. | Kwa kuwa umetwaa dhamana kwa nduguyo bure, Na kuwavua nguo zao walio uchi. |
| 7. | Hukumpa maji ya kunywa huyo aliyechoka, Nawe umemnyima chakula huyo mwenye njaa. |
| 8. | Lakini huyo shujaa, nchi ilikuwa yake; Na huyo mwenye kusifiwa, yeye aliikaa. |
| 9. | Umewafukuza wanawake wajane hali ya utupu, Na mikono ya mayatima imevunjwa. |
| 10. | Kwa hiyo umezungukwa na mitego, Na hofu ya ghafula yakutaabisha, |
| 11. | Au je! Huoni giza, Na maji mengi yanayokufunika? |
| 12. | Je! Mungu hayuko mbinguni juu? Tena tazama umbali wa nyota, jinsi zilivyo juu! |
| 13. | Nawe wasema, Mungu anajua nini? Je! Aweza kuamua kati ya giza kuu? |
| 14. | Mawingu mazito ni kifuniko chake, hata asione; Naye yuatembea juu ya kuba ya mbingu. |
| 15. | Je! Utaiandama njia ya zamani Waliyoikanyaga watu waovu? |
| 16. | Ambao walinyakuliwa kabla ya wakati wao, Msingi wao ulimwagika kama kijito cha maji; |
| 17. | Waliomwambia Mungu, Tuondokee; Tena, Huyo Mwenyezi aweza kutufanyia nini? |
| 18. | Naye ndiye aliyezijaza nyumba zao vitu vyema; Lakini mashauri ya waovu na yawe mbali nami. |
| 19. | Wenye haki huyaona hayo wakafurahi; Nao wasio na hatia huwacheka; |
| 20. | Wasema, Hakika hao waliotuinukia wamekatiliwa mbali, Na mabaki yao moto umeyateketeza. |
| 21. | Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia. |
| 22. | Uyapokee, tafadhali, mafunzo yatokayo kinywani mwake, Na maneno yake yaweke moyoni mwako. |
| 23. | Ukimrudia Mwenyezi, utajengwa; Ukiuondoa udhalimu mbali na hema yako. |
| 24. | Nawe hazina zako ziweke mchangani, Na dhahabu ya Ofiri iweke kati ya mawe ya vijito; |
| 25. | Naye Mwenyezi atakuwa hazina yako, Atakuwa ni fedha ya thamani kwako. |
| 26. | Kwani ndipo utakapojifurahisha katika Mwenyezi, Na kuinua uso wako kumwelekea Mungu. |
| 27. | Utamwomba yeye naye atakusikia; Nawe utazitimiliza nadhiri zako. |
| 28. | Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; Na mwanga utaziangazia njia zako. |
| 29. | Hapo watakapokuangusha, utasema, Kuna kuinuka tena; Naye mnyenyekevu Mungu atamwokoa. |
| 30. | Atamwokoa na huyo asiye na hatia; Naam, utaokolewa kwa sababu ya usafi wa mikono yako. |
| ← Job (22/42) → |