| ← Job (21/42) → |
| 1. | Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, |
| 2. | Yasikizeni sana maneno yangu; Jambo hili na liwe faraja yenu. |
| 3. | Niacheni, nami pia nitanena; Tena nikiisha nena, zidini kudhihaki. |
| 4. | Mimi, je! Mashitaka yangu yamhusu mwanadamu? Nami kwa nini nisikose kusubiri? |
| 5. | Niangalieni, mkastaajabu, Mkaweke mkono kinywani. |
| 6. | Hata nikumbukapo nahuzunika, Na utisho wanishika mwilini mwangu. |
| 7. | Mbona waovu wanaishi, Na kuwa wazee, naam, na kuongezeka kuwa na nguvu? |
| 8. | Kizazi chao kinathibitika nao machoni pao, Na wazao wao mbele ya macho yao. |
| 9. | Nyumba zao zi salama pasina hofu, Wala fimbo ya Mungu haiwapigi. |
| 10. | Fahali wao huvyaza wala hapungukiwi na nguvu; Ng'ombe wao mke huzaa, asiharibu mimba. |
| 11. | Huwatoa kama kundi watoto wao. Na watoto wao hucheza. |
| 12. | Huimba kwa matari na kwa kinubi, Na kuifurahia sauti ya filimbi. |
| 13. | Siku zao hutumia katika kufanikiwa, Kisha hushuka kuzimuni ghafula. |
| 14. | Walakini walimwambia Mungu. Tuondokee; Kwani hatutaki kuzijua njia zako. |
| 15. | Huyo Mwenyezi ni nani, hata tumtumikie? Nasi tutafaidiwa nini tukimwomba? |
| 16. | Tazama, kufanikiwa kwao hakumo mkononi mwao; Mashauri ya waovu na yawe mbali nami. |
| 17. | Je! Ni mara ngapi taa yao waovu huzimishwa? Na msiba wao kuwajilia? Na Mungu kuwagawanyia uchungu kwa hasira yake? |
| 18. | Ili wawe kama mabua makavu mbele ya upepo, Kama makapi yaliyochukuliwa na dhoruba? |
| 19. | Mwasema, Mungu huwawekea watoto wa mtu huo uovu wake. Na amlipe mwenyewe, ili apate kuujua. |
| 20. | Macho yake mwenyewe na yaone uharibifu wake, Akanywe ghadhabu zake Mwenyezi. |
| 21. | Kwani ana furaha gani katika mbari yake baada yake, Hesabu ya miezi yake itakapokwisha katwa katikati? |
| 22. | Je! Mtu awaye yote atamfundisha Mungu maarifa? Naye ndiye awahukumuye walioko juu. |
| 23. | Mmoja hufa katika nguvu zake kamili, Mwenye kukaa salama na kustarehe; |
| 24. | Vyombo vyake vimejaa maziwa, Na mafuta ya mifupani mwake ni laini. |
| 25. | Mwingine hufa katika uchungu wa roho, Asionje mema kamwe. |
| 26. | Wao hulala mavumbini sawasawa, Mabuu huwafunika. |
| 27. | Tazama, nayajua mawazo yenu, Na mashauri mnayoazimia kwa uovu juu yangu. |
| 28. | Kwa kuwa mwasema, Nyumba ya huyo mkuu i wapi? Na hema waliyoikaa hao waovu i wapi? |
| 29. | Je! Hamkuwauliza wapitao njiani? Na maonyo yao hamyajui? |
| 30. | Kwamba mwovu huachiliwa katika siku ya msiba? Na kuongozwa nje katika siku ya ghadhabu? |
| 31. | Ni nani atakayetangaza njia yake usoni pake? Tena ni nani atakayemlipa kwa hayo aliyofanya? |
| 32. | Pamoja na hayo atachukuliwa kaburini, Nao watalinda zamu juu ya ziara lake. |
| 33. | Udongo wa bondeni utakuwa tamu kwake, Na watu wote watafuata nyuma yake, Kama vile walivyomtangulia watu wasiohesabika. |
| 34. | Basi imekuwaje ninyi kunituza moyo bure, Kwa kuwa katika jawabu zenu unasalia uongo tu. |
| ← Job (21/42) → |