| ← Job (19/42) → |
| 1. | Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, |
| 2. | Je! Mtanichukiza nafsi yangu hata lini, Na kunivunja-vunja kwa maneno? |
| 3. | Mara kumi hizi mmenishutumu; Hamwoni haya kunifanyia mambo magumu. |
| 4. | Ingawaje nimekosa, Kosa langu hukaa kwangu mwenyewe. |
| 5. | Kwamba mtajitukuza juu yangu, Na kunena juu yangu shutumu langu; |
| 6. | Jueni basi kuwa Mungu amenipotosha, Na kunizingira kwa wavu wake. |
| 7. | Tazama, nalia, Udhalimu, lakini sisikiwi; Naulilia msaada, wala hapana hukumu. |
| 8. | Yeye ameiziba njia yangu nisipate kupita, Na kutia giza katika mapito yangu. |
| 9. | Amenivua utukufu wangu, Na kuiondoa taji kichwani mwangu. |
| 10. | Amenibomoa pande zote, nami nimetoweka; Na tumaini langu ameling'oa kama mti. |
| 11. | Tena ameziwasha ghadhabu zake juu yangu, Akanihesabia kuwa mmoja katika watesi wake. |
| 12. | Majeshi yake husongea pamoja, na kunipandishia njia yao, Na kupiga marago kuizunguka hema yangu. |
| 13. | Amewaweka ndugu zangu mbali nami, Na wanijuao wametengwa nami kabisa. |
| 14. | Watu wa mbari yangu wamekoma, Na rafiki zangu niwapendao wamenisahau. |
| 15. | Wakaao nyumbani mwangu, na vijakazi vyangu, wanihesabu kuwa mgeni; Mimi ni mgeni machoni pao. |
| 16. | Namwita mtumishi wangu, wala haniitikii, Ingawa namsihi kwa kinywa changu. |
| 17. | Pumzi zangu ni kama za mgeni kwa mke wangu, Nami ni machukizo kwa ndugu zangu. |
| 18. | Hata watoto wadogo hunidharau; Nikiondoka, huninena. |
| 19. | Wasiri wangu wote wanichukia; Na hao niliowapenda wamenigeukia. |
| 20. | Mfupa wangu unagandamana na ngozi yangu na nyama yangu, Nami nimeokoka na ngozi ya meno yangu tu. |
| 21. | Nihurumieni, nihurumieni, enyi rafiki zangu, Kwa maana mkono wa Mungu umenigusa. |
| 22. | Mbona ninyi mnaniudhi kama Mungu, Wala hamkutosheka na nyama yangu? |
| 23. | Laiti maneno yangu yangeandikwa sasa! Laiti yangeandikwa kitabuni! |
| 24. | Yakachorwa katika mwamba milele, Kwa kalamu ya chuma na risasi. |
| 25. | Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi. |
| 26. | Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu; |
| 27. | Nami nitamwona mimi nafsi yangu, Na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine. |
| 28. | Kama mkisema, Jinsi tutakavyomwudhi! Kwa kuwa shina la jambo hili limeonekana kwake; |
| 29. | Uogopeni upanga; Kwa maana adhabu za upanga zina ghadhabu, Mpate kujua ya kwamba hukumu iko. |
| ← Job (19/42) → |