| ← Job (18/42) → |
| 1. | Ndipo Bildadi, Mshuhi, akajibu, na kusema, |
| 2. | Je! Hata lini utayategea maneno mitambo? Fikiri, kisha baadaye tutanena. |
| 3. | Twahesabiwa kuwa wanyama kwa sababu gani, Tena kuwa wanajisi machoni pako? |
| 4. | Wewe ujiraruaye mwenyewe katika hasira yako, Je! Dunia itaachwa kwa ajili yako wewe? Au jabali litaondolewa mahali pake? |
| 5. | Naam, mwanga wa waovu utazimika, Wala mwali wa moto wake hautang'aa. |
| 6. | Mwanga hemani mwake utakuwa giza, Nayo taa iliyo juu yake itazimishwa. |
| 7. | Hatua zake za nguvu zitasongwa, Na shauri lake mwenyewe litamwangusha chini. |
| 8. | Kwani ametupwa katika wavu na miguu yake mwenyewe, Naye huenda juu ya matanzi. |
| 9. | Tanzi litamshika kisigino chake, Na mtambo utamgwia. |
| 10. | Amefichiwa tanzi chini, Na mtego amewekewa njiani. |
| 11. | Matisho yatamtia hofu pande zote, Na kumfukuza karibu na visigino vyake. |
| 12. | Nguvu zake zitaliwa na njaa, Na msiba utakuwa tayari kwa kusita kwake. |
| 13. | Utakula via vya mwili wake, Naam, mzaliwa wa kwanza wa mauti atavila via vyake. |
| 14. | Atang'olewa katika hema yake aliyokuwa akiitumaini; Naye atapelekwa kwake mfalme wa utisho. |
| 15. | Ambacho si chake kitakaa katika hema yake; Kiberiti kitamwagwa juu ya makazi yake. |
| 16. | Chini, mizizi yake itakaushwa; Na juu, tawi lake litasinyaa. |
| 17. | Kumbukumbu lake litakoma katika nchi, Wala hatakuwa na jina mashambani. |
| 18. | Atakimbizwa kutoka mwangani hata gizani, Na kufukuzwa atoke duniani. |
| 19. | Hatakuwa na mwana wala mjukuu kati ya watu wake, Wala hatasalia mtu hapo alipokaa. |
| 20. | Hao wanaokaa magharibi watastaajabia siku yake, Kama vile wanaokaa mashariki walivyotiwa hofu. |
| 21. | Hakika ndivyo yalivyo makazi ya wapotovu, Na hapa ni mahali pake asiyemjua Mungu. |
| ← Job (18/42) → |