← Job (15/42) → |
1. | Ndipo Elifazi, Mtemani, akajibu, na kusema, |
2. | Je! Yapasa mtu mwenye hekima kujibu kwa ujuzi wa uvuvio, Na kujaza tumbo lake na upepo wa mashariki? |
3. | Je! Ahoji na mazungumzo yasiyo faida, Au kwa maneno ambayo hawezi kufanya mema kwayo? |
4. | Naam, wewe waondoa kicho, Nawe wazuia ibada mbele za Mungu. |
5. | Kwani uovu wako unakufundisha kinywa chako, Nawe wachagua ulimi wake mwenye hila. |
6. | Kinywa chako mwenyewe chakuhukumia makosa, wala si mimi; Naam, midomo yako mwenyewe hushuhudia juu yako. |
7. | Je! Wewe u mtu wa kwanza aliyezaliwa? Au, ulizawa wewe kabla ya milima? |
8. | Je! Umesikia mashauri ya siri ya Mungu? Nawe je! Wazuia hekima iwe yako tu? |
9. | Je! Wewe wajua neno lipi, ambalo sisi hatulijui? Nawe wafahamu nini, ambalo halimo ndani yetu? |
10. | Wenye mvi, na walio wazee sana, wote wapo pamoja nasi, Ambao ni wazee kuliko baba yako. |
11. | Je! Utulizi wa Mungu ni mdogo sana kwako, Na hilo neno la upole si kitu kwako? |
12. | Mbona moyo wako unakutaharakisha! Na macho yako, je! Kwani kung'ariza? |
13. | Hata ukageuza roho yako iwe kinyume cha Mungu, Na kuyatoa maneno kama hayo kinywani mwako. |
14. | Je! Mwanadamu ni kitu gani, hata akawa safi? Huyo aliyezaliwa na mwanamke, hata awe na haki? |
15. | Yeye hawategemei watakatifu wake; Naam, mbingu nazo si safi machoni pake. |
16. | Sembuse mtu ambaye ni mwenye kuchukiza na uchafu, Mwanadamu anywaye uovu kama anywavyo maji! |
17. | Mimi nitakuonyesha, unisikilize; Na hayo yote niliyoyaona nitayanena; |
18. | (Ambayo watu wenye hekima wameyatangaza Tokea baba zao, wala hawakuyaficha; |
19. | Waliopewa hiyo nchi peke yao, Wala mgeni hakupita kati yao); |
20. | Mtu mwovu huwa na uchungu siku zake zote, Hata hesabu ya miaka aliyowekewa mwenye kuonea. |
21. | Sauti za utisho zi masikioni mwake; Katika kufanikiwa kwake mtekaji nyara atamjia juu yake; |
22. | Yeye hasadiki kwamba atarudi kutoka gizani, Naye hungojewa na upanga; |
23. | Hutanga-tanga ili apate chakula, akisema, Ki wapi? Ajua kwamba siku ya giza i tayari karibu yake; |
24. | Mateso na dhiki humtia hofu; Humshinda kama vile mfalme aliye tayari kwa vita; |
25. | Kwa kuwa amenyosha mkono wake juu ya Mungu, Na kuendelea kwa kiburi kinyume cha Mwenyezi; |
26. | Humshambulia na shingo ngumu, Kwa mafundo makubwa ya ngao zake; |
27. | Kwa kuwa amefunika uso wake na kunona kwake, Na kuwandisha mafuta kiunoni mwake; Naye amekaa katika miji iliyo ukiwa, |
28. | Katika nyumba ambazo hapana mtu azikaaye, Zilizokuwa tayari kuwa magofu. |
29. | Hatakuwa tajiri, wala mali zake hazitadumu, Wala maongeo yao hayatainama nchi. |
30. | Hataondoka gizani; Ndimi za moto zitayakausha matawi yake, Naye ataondoka kwa pumzi za kinywa chake. |
31. | Asiutumainie ubatili, na kujidanganya; Kwa kuwa huo ubatili ndio utakaokuwa ujira wake. |
32. | Jambo hili litatendeka kabla ya wakati wake, Na tawi lake halitasitawi. |
33. | Atayapukutisha mapooza yake kama mzabibu, Na kuyatupa maua yake kama mzeituni. |
34. | Kwa kuwa jamii ya hao wasiomcha Mungu watakuwa tasa, Na moto utateketeza mahema yenye rushwa. |
35. | Wao hutunga mimba ya madhara, na kuzaa uovu, Nalo tumbo lao hutengeza udanganyifu. |
← Job (15/42) → |