| ← Job (14/42) → |
| 1. | Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. |
| 2. | Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe. |
| 3. | Nawe, je! Wafumbua macho yako kumwangalia mtu kama yeye, Na kunitia katika hukumu pamoja nawe? |
| 4. | Ni nani awezaye kutoa kitu kilicho safi kitoke katika kitu kichafu? Hapana awezaye. |
| 5. | Kwa kuwa siku zake zimeamriwa, hesabu ya miezi yake unayo wewe, Nawe umemwekea mipaka yake asiyoweza kuipita; |
| 6. | Acha kumwangalia yeye, apate kupumzika, Hata atakapoitimiza siku yake, kama aliyeajiriwa. |
| 7. | Kwani yako matumaini ya mti, ya kuwa ukikatwa utachipuka tena, Wala machipukizi yake hayatakoma. |
| 8. | Ijapokuwa mizizi yake huchakaa mchangani, Na shina lake kufa katika udongo; |
| 9. | Lakini kwa harufu ya maji utachipuka, Na kutoa matawi kama mche. |
| 10. | Lakini mwanadamu hufa, huifariki dunia; Naam, mwanadamu hutoa roho, naye yupo wapi? |
| 11. | Kama vile maji kupwa katika bahari, Na mto kupunguka na kukatika; |
| 12. | Ni vivyo mwanadamu hulala chini, asiinuke; Hata wakati wa mbingu kutokuwako tena, hawataamka, Wala kuamshwa usingizini. |
| 13. | Laiti ungenificha kuzimuni, Ukanilinda kwa siri, hata ghadhabu zako zitakapopita, Na kuniandikia muda ulioamriwa, na kunikumbuka! |
| 14. | Mtu akifa, je! Atakuwa hai tena? Mimi ningengoja siku zote za vita vyangu, Hata kufunguliwa kwangu kunifikilie. |
| 15. | Wewe ungeita, nami ningekujibu; Ungekuwa na tamaa ya kazi ya mikono yako. |
| 16. | Lakini sasa wazihesabu hatua zangu; Je! Huchungulii dhambi yangu? |
| 17. | Kosa langu limetiwa muhuri mfukoni, Nawe waufunga uovu wangu. |
| 18. | Lakini, tazama, mlima ukianguka hutoweka, Nalo jabali huondolewa mahali pake; |
| 19. | Maji mengi huyapunguza mawe; Mafuriko yake huuchukua mchanga wa nchi; Nawe matumaini ya wanadamu wayaangamiza. |
| 20. | Wewe wamshinda nguvu sikuzote, naye hupita aende zake Wabadili sura zake, na kumpeleka aondoke. |
| 21. | Wanawe hufikilia heshima, wala yeye hajui; Kisha wao huaibishwa, lakini yeye hana habari zao. |
| 22. | Lakini mwili ulio juu yake una maumivu, Na nafsi yake ndani huomboleza. |
| ← Job (14/42) → |