← Job (12/42) → |
1. | Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, |
2. | Hapana shaka ninyi ndinyi watu halisi, Nanyi mtakapokufa, ndipo na hekima itakoma. |
3. | Lakini mimi pia, nina fahamu kama ninyi; Mimi si duni yenu ninyi; Naam, ni nani asiyejua mambo kama hayo? |
4. | Mimi ni mtu wa kuchekwa na jirani yake, Ni mtu niliyemwita Mungu, naye akanijibu; Huyo mwenye haki, aliye mtimilifu, amekuwa ni kicheko. |
5. | Katika mawazo yake huyo aliye na raha mna kudharau mashaka; Tayari kwa ajili ya wenye kuteleza miguu. |
6. | Hema za wapokonyi hufanikiwa, Na hao wamkasirishao Mungu hukaa salama; Mikononi mwao Mungu huleta vitu vingi. |
7. | Lakini sasa waulize hao wanyama, nao watakufundisha; Na nyuni wa angani, nao watakuambia; |
8. | Au nena na nchi, nayo itakufundisha; Nao samaki wa baharini watakutangazia. |
9. | Katika hawa wote ni yupi asiyejua, Kwamba ni mkono wa Bwana uliofanya haya? |
10. | Ambaye nafsi ya kila kilicho hai i mkononi mwake, Na pumzi zao wanadamu wote. |
11. | Je! Sikio silo lijaribulo maneno, Kama vile kaakaa lionjavyo chakula? |
12. | Wazee ndio walio na hekima, Na katika kuishi siku nyingi iko fahamu. |
13. | Hekima na amri zina yeye [Mungu]; Yeye anayo mashauri na fahamu. |
14. | Tazama, yuavunja, wala haiwezekani kujenga tena; Humfunga mtu, wala haiwezekani kumfungua. |
15. | Tazama, yuayazuia maji, nayo yakatika; Tena, huyapeleka, nayo yaipindua dunia. |
16. | Kwake yeye ziko nguvu, na makusudi kufanikiwa; Huyo adanganywaye, na mdanganyi pia ni wake. |
17. | Yeye huwaondoa washauri hali wametekwa nyara, Naye huwafanya waamuzi kuwa ni wapumbavu. |
18. | Yeye hulegeza kifungo cha wafalme, Na kuwafunga viuno vyao kwa mshipi. |
19. | Yeye huwaondoa makuhani hali wametekwa nyara. Na kuwapindua mashujaa. |
20. | Huondoa matamko ya hao walioaminiwa, Na kuondoa fahamu za wazee. |
21. | Humwaga aibu juu ya hao wakuu, Na kulegeza mshipi wa wenye nguvu. |
22. | Huvumbua mambo ya siri tokea gizani, Na hicho kilicho giza tupu huleta mwangani. |
23. | Huyaongeza mataifa, na kuyaangamiza; Huyaeneza mataifa mbali, na kuyaacha. |
24. | Huwaondolea moyo wakuu wa watu wa nchi, Na kuwapoteza nyikani pasipokuwa na njia. |
25. | Wao hupapasa gizani pasipokuwa na mwanga, Naye huwafanya kupepesuka kama vile mlevi. |
← Job (12/42) → |