Jeremiah (8/52)  

1. Wakati ule, asema Bwana, watatoa mifupa ya wafalme wa Yuda, na mifupa ya wakuu wake, na mifupa ya makuhani, na mifupa ya manabii na mifupa ya wenyeji wa Yerusalemu, itoke makaburini mwao;
2. nao wataitawanya mbele ya jua, na mwezi, na jeshi lote la mbinguni, walivyovipenda, na kuvitumikia, na kuandamana navyo, na kuvitafuta, na kuviabudu haitakusanywa pamoja tena, wala kuzikwa; itakuwa ni samadi juu ya uso wa nchi.
3. Na kufa kutachaguliwa kuliko kuishi na mabaki yote waliosalia katika jamaa hii mbovu, waliosalia kila mahali nilikowafukuza, asema Bwana wa majeshi.
4. Tena utawaambia, Bwana asema hivi, Je! Watu wataanguka, wasisimame tena? Je! Mtu atageuka aende zake, asirudi tena?
5. Mbona, basi, watu hawa wa Yerusalemu wamegeuka waende nyuma, wasikome kugeuka hivyo? Hushika udanganyifu sana, hukataa kurudi.
6. Nalisikiliza nikasikia, lakini walisema yasiyo sawa; hapana mtu aliyetubia maovu yake, akisema, Nimefanya nini? Kila mtu hurudia mwendo wake mwenyewe, kama farasi aendavyo kasi vitani.
7. Naam, koikoi angani ajua nyakati zake zilizoamriwa; na hua na mbayuwayu na korongo huangalia wakati wa kuja kwao; bali watu wangu hawazijui amri za Bwana.
8. Mwasemaje, Sisi tuna akili, na torati ya Bwana tunayo pamoja nasi? Lakini, tazama, kalamu yenye uongo ya waandishi imeifanya kuwa uongo.
9. Wenye hekima wametahayari, wamefadhaika na kushikwa; tazama, wamelikataa neno la Bwana, wana akili gani ndani yao?
10. Basi, kwa hiyo nitawapa watu wengine wake zao na mashamba yao nitawapa wale watakaowamiliki; maana kila mmoja wao, tangu aliye mdogo hata aliye mkubwa, ni mtamanifu; tangu nabii hata kuhani, kila mmoja hutenda mambo ya udanganyifu.
11. Kwa maana wameiponya jeraha ya binti ya watu wangu kwa juu-juu tu, wakisema, Amani, Amani, wala hapana amani.
12. Je! Walitahayarika, walipokuwa wametenda machukizo? La! Hawakutahayarika, wala hawakuweza kuona haya usoni; basi wataanguka miongoni mwao waangukao; wakati wa kujiliwa kwao wataangushwa chini, asema Bwana.
13. Nitawaangamiza kabisa, asema Bwana; hapana zabibu katika mizabibu, wala tini katika mitini, hata jani lake litanyauka; na vitu vile nilivyowapa vitawapotea.
14. Mbona tunakaa kimya? Jikusanyeni, tukaingie ndani ya miji yenye maboma, tukanyamaze humo kwa maana Bwana, Mungu wetu, ametunyamazisha, naye ametupa maji yenye uchungu tunywe, kwa sababu tumemwasi Bwana.
15. Tulitazamia amani, lakini hayakuja mema yo yote; tulitazamia wakati wa kupona, na tazama, kufadhaika tu!
16. Kutoka Dani kumesikiwa mkoromo wa farasi zake; nchi yote pia inatetemeka kwa sauti ya mlio wa farasi zake za vita; maana wamekuja, wamekula nchi na vyote vilivyomo; huo mji na wote wakaao ndani yake.
17. Maana, tazama, nitatuma nyoka, naam, fira, kati yenu, wasioweza kutumbuizwa kwa uganga; nao watawauma, asema Bwana.
18. Laiti ningeweza kujifariji, nisione huzuni! Moyo wangu umezimia ndani yangu.
19. Tazama, sauti ya kilio cha binti ya watu wangu, itokayo katika nchi iliyo mbali sana; Je! Bwana hayumo katika Sayuni? Mfalme wake hayumo ndani yake? Mbona wamenikasirisha kwa sanamu zao walizochonga, na kwa ubatili wa kigeni?
20. Mavuno yamepita, wakati wa hari umekwisha, wala sisi hatukuokoka.
21. Kwa sababu ya maumivu ya binti ya watu wangu nimeumia mimi; nimevaa kaniki; ushangao umenishika.
22. Je! Hapana zeri katika Gileadi? Huko hakuna tabibu? Mbona, basi, haijarejea afya ya binti ya watu wangu?

  Jeremiah (8/52)