← Jeremiah (6/52) → |
1. | Kimbieni mpate kuwa salama, enyi wana wa Benyamini; tokeni katika Yerusalemu, pigeni tarumbeta katika Tekoa, simamisheni ishara juu ya Beth-hakeremu; kwa maana mabaya yanachungulia toka kaskazini, na uharibifu mkuu. |
2. | Binti Sayuni aliye mzuri, mwororo, nitamkatilia mbali. |
3. | Wachungaji na makundi yao ya kondoo watamjilia; watapiga hema zao karibu naye pande zote; watalisha kila mmoja mahali pake. |
4. | Takaseni vita juu yake; inukeni, na tupande juu wakati wa adhuhuri. Ole wetu, kwa kuwa mchana umeanza kupungua, vivuli vya jioni vinazidi kuwa virefu. |
5. | Inukeni, na tupande juu wakati wa usiku, tukayaharibu majumba yake. |
6. | Maana Bwana wa majeshi asema hivi, Jikatieni miti, mfanyize boma juu ya Yerusalemu. Mji huu ni mji unaojiliwa; dhuluma tupu imo ndani yake. |
7. | Kama vile kisima kitoavyo maji yake, ndivyo utoavyo uovu wake; jeuri na kuharibu kwasikiwa ndani yake; ugonjwa na jeraha zi mbele zangu daima. |
8. | Uadhibishwe, Ee Yerusalemu, nafsi yangu, isije ikafarakana nawe; nisije nikakufanya ukiwa, nchi isiyokaliwa na watu. |
9. | Bwana wa majeshi asema hivi, Wataokota mabaki ya Israeli kama mzabibu; rudisha mkono wako ndani ya vikapu, kama mchuma zabibu. |
10. | Niseme na nani na kushuhudia, wapate kusikia? Tazama, sikio lao halikutahiriwa, wala hawawezi kusikiliza; tazama, neno la Bwana limekuwa matukano kwao; hawalifurahii. |
11. | Lakini nimejaa ghadhabu ya Bwana; nimechoka kwa kujizuia; imwageni juu ya watoto walio njiani, na juu ya kusanyiko la vijana pia; maana hata mume atatwaliwa pamoja na mkewe, mzee pamoja na yeye aliyetimiza siku zake. |
12. | Na nyumba zao zitakuwa mali za watu wengine, mashamba yao na wake zao pamoja; kwa kuwa nitaunyosha mkono wangu juu ya wenyeji wa nchi hii, asema Bwana. |
13. | Kwa maana, tangu aliye mdogo hata aliye mkubwa miongoni mwao, kila mmoja ni mtamanifu; na, tangu nabii hata kuhani, kila mmoja hutenda mambo ya udanganyifu. |
14. | Wameiponya jeraha ya watu wangu kwa juu juu tu, wakisema, Amani, Amani, wala hapana amani. |
15. | Je! Walitahayarika, walipokuwa wameunda machukizo? La, hawakutahayarika hata kidogo, wala hawakuweza kuona haya usoni; basi, wataanguka miongoni mwa hao waangukao; wakati nitakapowajilia wataangushwa chini, asema Bwana. |
16. | Bwana asema hivi, Simameni katika njia kuu, mkaone, mkaulize habari za mapito ya zamani, I wapi njia iliyo njema? Mkaende katika njia hiyo, nanyi mtajipatia raha katika nafsi zenu. Lakini walisema, Hatutaki kwenda katika njia hiyo. |
17. | Nami naliweka walinzi juu yenu, wakisema, Isikilizeni sauti ya tarumbeta; lakini walisema, Hatutaki kusikiliza. |
18. | Kwa sababu hiyo sikilizeni, enyi mataifa, mkajue, Ee kusanyiko, ni jambo gani litokealo kati yao. |
19. | Sikia, Ee nchi; tazama, nitaleta mabaya juu ya watu hawa, naam, matunda ya mawazo yao, kwa sababu hawakuyasikiliza maneno yangu; tena kwa habari ya sheria yangu, wameikataa. |
20. | Yafaa nini niletewe ubani kutoka Sheba, na uudi kutoka nchi iliyo mbali? Sadaka zenu za kuteketezwa hazikubaliwi, wala dhabihu zenu haziniridhii. |
21. | Basi, kwa hiyo, Bwana asema hivi, Tazama, nitaweka makwazo mbele ya watu hawa, na baba na wana wao watajikwaa pamoja; jirani ya mtu na rafiki yake watapotea. |
22. | Bwana asema hivi, Tazama, watu wanakuja, wakitoka katika nchi ya kaskazini; na taifa kubwa litaamshwa, litokalo katika pande za mwisho wa dunia. |
23. | Washika upinde na mkuki; ni wakatili, hawana huruma; sauti yao huvuma kama bahari, nao wamepanda farasi zao; kila mmoja kama mtu wa vita amejipanga juu yako, Ee binti Sayuni. |
24. | Tumesikia habari zake; mikono yetu inalegea; dhiki imetushika, na utungu kama wa mwanamke wakati wa kuzaa kwake. |
25. | Msitoke kwenda mashambani, wala msitembee njiani, kwa maana upanga wa adui uko huko; hofu ziko pande zote. |
26. | Ee binti wa watu wangu, ujivike nguo ya magunia, na kugaagaa katika majivu; fanya maombolezo, kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, maombolezo ya uchungu mwingi; maana mwenye kuteka nyara atakuja juu yetu ghafula. |
27. | Nimekuweka uwe mnara na ngome kati ya watu wangu; upate kuijua njia yao na kuijaribu. |
28. | Ni waasi kupita kiasi wote pia, waendao huko na huko wakisingizia, ni shaba na chuma hao, hutenda dhuluma wote pia. |
29. | Mifuo inafukuta kwa nguvu; risasi tu inatoka katika moto huo; mfua fedha ameyeyusha bure tu; maana wabaya hawaondolewi mbali. |
30. | Watu watawaita taka za fedha, kwa sababu Bwana amewakataa. |
← Jeremiah (6/52) → |