| ← Jeremiah (49/52) → |
| 1. | Habari za wana wa Amoni. Bwana asema hivi, Je, Israeli hana wana? Je! Hana mrithi? Basi, mbona Malkamu anamiliki Gadi, na watu wake wanakaa katika miji yake? |
| 2. | Basi, kwa sababu hiyo, tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakaposikizisha mshindo wa vita juu ya Raba, mji wa Amoni, nao utakuwa magofu ya ukiwa, na binti zake watateketezwa kwa moto; ndipo Israeli watawamiliki wao waliokuwa wakimmiliki, asema Bwana. |
| 3. | Piga yowe, Ee Heshboni, Kwa maana Ai umeangamizwa; Lieni, enyi binti za Raba, Mjivike nguo za magunia; Ombolezeni, mkipiga mbio Huko na huko kati ya maboma; Maana Malkamu atakwenda kuhamishwa, Makuhani wake na wakuu wake pamoja. |
| 4. | Mbona unajisifu kwa sababu ya mabonde, bonde lako litiririkalo, Ee binti mwenye kuasi? Utumainiaye hazina zako, ukisema, Ni nani atakayenijilia? |
| 5. | Tazama, nitaleta hofu juu yako, asema Bwana, Bwana wa majeshi, itakayotoka kwa wote wakuzungukao; nanyi mtafukuzwa nje, kila mtu mbali kabisa, wala hapana mtu wa kuwakusanya wapoteao. |
| 6. | Lakini baada ya hayo nitawarudisha wana wa Amoni walio utumwani, asema Bwana. |
| 7. | Habari za Edomu. Bwana wa majeshi asema hivi, Je! Hapana tena hekima katika Temani? Mashauri yamewapotea wenye busara? Je! Imetoweka hekima yao? |
| 8. | Kimbieni, rudini nyuma, kaeni chini sana, enyi mnaokaa Dedani; maana nitaleta msiba wa Esau juu yake, wakati nitakapomwangalia. |
| 9. | Je! Kama wachuma zabibu wangekujia, wasingeacha zabibu ziokotwe? Kama wangekujia wevi usiku, wasingeharibu hata watakapopata vya kutosha? |
| 10. | Lakini nimemwacha Esau hana kitu, nimepafunua mahali pake pa siri, wala hataweza kujificha; kizazi chake kimeangamizwa, na ndugu zake, na jirani zake, naye mwenyewe hayuko. |
| 11. | Waache watoto wako wasio na baba, mimi nitawahifadhi hai, na wajane wako na wanitumaini mimi. |
| 12. | Maana Bwana asema hivi, Tazama, wale wasioandikiwa kunywea kikombe, watakinywea, ni hakika; na wewe je! U mtu ambaye hataadhibiwa kabisa? Hukosi utaadhibiwa, naam, kunywa utakunywa. |
| 13. | Kwa maana nimeapa kwa nafsi yangu, asema Bwana, kwamba Bozra utakuwa ajabu, na aibu, na ukiwa, na laana; na miji yake yote itakuwa ukiwa wa daima. |
| 14. | Nimepata habari kwa Bwana, Na mjumbe ametumwa kati ya mataifa, Akisema, Jikusanyeni, mkaujie, Mkainuke kwenda vitani. |
| 15. | Maana nimekufanya mdogo kati ya mataifa, Na kudharauliwa katika watu. |
| 16. | Katika habari za kuogofya kwako, Kiburi cha moyo wako kimekudanganya, Wewe ukaaye katika pango za majabali, Ushikaye kilele cha milima; Ujapofanya kioto chako juu sana kama tai, Nitakushusha kutoka huko; asema Bwana. |
| 17. | Na Edomu atakuwa ajabu; kila mtu apitaye atashangaa, na kuzomea, kwa sababu ya mapigo yake yote. |
| 18. | Kama vile vilivyotokea wakati wa kuangushwa Sodoma na Gomora, na miji iliyokuwa karibu nayo, asema Bwana; hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama mgeni akaavyo. |
| 19. | Angalia, atapanda kama simba toka kiburi cha Yordani juu ya malisho yasiyonyauka; lakini nitamkimbiza ghafula ayaache; na yeye aliye mteule nitamweka juu yake; maana ni nani aliye kama mimi? Tena ni nani atakayeniandikia muda? Tena ni mchungaji yupi atakayesimama mbele zangu? |
| 20. | Basi, lisikieni shauri la Bwana; Alilolifanya juu ya Edomu; Na makusudi yake aliyoyakusudia Juu yao wakaao Temani; Hakika watawaburura, naam, wadogo wa kundi; Hakika malisho yao yatafadhaika kwa ajili yao. |
| 21. | Nchi yatetemeka kwa sauti ya kuanguka kwao; Kuna kilio, sauti yake yasikiwa katika Bahari ya Shamu. |
| 22. | Tazama, atapanda na kuruka kama tai, na kutandaza mabawa yake juu ya Bozra; na mioyo ya mashujaa wa Edomu siku hiyo itakuwa kama moyo wa mwanamke katika utungu wake. |
| 23. | Habari za Dameski. Hamathi umetahayarika, na Arpadi pia; Maana wamesikia habari mbaya; Wameyeyuka kabisa; Huzuni iko baharini, haiwezi kutulia. |
| 24. | Dameski umedhoofika; Umejigeuza kukimbia; tetemko limeushika; Dhiki na huzuni zimeupata, Kama za mwanamke katika utungu wake. |
| 25. | Imekuwaje mji wa sifa haukuachwa, mji wa furaha yangu? |
| 26. | Kwa hiyo vijana wake wataanguka katika njia kuu zake, na watu wote wa vita watanyamazishwa katika siku hiyo, asema Bwana wa majeshi. |
| 27. | Nami nitawasha moto katika ukuta wa Dameski, nao utayateketeza majumba ya Ben-hadadi. |
| 28. | Habari za Kedari, na za falme za Hazori, ambazo Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alizipiga. Bwana asema hivi, Ondokeni, pandeni hata Kedari, mkawateke nyara wana wa mashariki. |
| 29. | Hema zao na makundi yao watayatwaa; watachukulia mbali mapazia yao kwa faida yao wenyewe, na vyombo vyao vyote, na ngamia zao; nao watawapigia kelele wakisema, Hofu ziko pande zote. |
| 30. | Kimbieni ninyi, enendeni mbali mkitanga-tanga, kaeni chini sana, enyi mkaao Hazori, asema Bwana; maana Nebukadreza, mfalme wa Babeli, amefanya shauri juu yenu, naye amekusudia neno juu yenu. |
| 31. | Ondokeni, pandeni hata taifa lililo katika hali ya raha, likaalo bila kuhangaika, asema Bwana; wasio na malango wala makomeo, wakaao peke yao. |
| 32. | Na ngamia zao watakuwa mateka, na wingi wa makundi yao utakuwa nyara; nami nitawatawanya hata pepo zote watu wale wanyoao denge; nami nitaleta msiba wao toka pande zao zote, asema Bwana. |
| 33. | Na Hazori utakuwa kao la mbwa-mwitu; ukiwa milele; hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama mgeni akaavyo. |
| 34. | Neno la Bwana lililomjia Yeremia, nabii, juu ya Elamu, mwanzo wa kumiliki kwake Sedekia, mfalme wa Yuda, kusema, |
| 35. | Bwana wa majeshi asema hivi, Tazama nitauvunja upinde wa Elamu, ulio mkuu katika nguvu zao. |
| 36. | Na juu ya Elamu nitazileta pepo nne, toka pembe nne za mbinguni, nami nitawatawanya hata pepo nne zote, wala hapana taifa ambalo hawatalifikilia watu wa Elamu waliofukuzwa. |
| 37. | Nami nitawafadhaisha watu wa Elamu mbele ya adui zao, na mbele ya hao wanaowatafuta roho zao; nami nitawaletea mabaya, naam, hasira yangu kali, asema Bwana; nami nitautuma upanga uwafuatie, hata nitakapowaangamiza; |
| 38. | nami nitaweka kiti changu cha enzi huko Elamu, nami nitawaharibu, mfalme na wakuu, watoke huko, asema Bwana. |
| 39. | Lakini itakuwa, katika siku za mwisho, nitawarudisha wafungwa wa Elamu, asema Bwana. |
| ← Jeremiah (49/52) → |