Jeremiah (42/52)  

1. Ndipo maakida wote wa majeshi, na Yohana, mwana wa Karea, na Yezania, mwana wa Hoshaya, na watu wote tangu wadogo hata wakubwa, wakakaribia,
2. wakamwambia Yeremia, nabii, Twakusihi, maombi yetu yakubaliwe mbele yako, ukatuombee kwa Bwana, Mungu wako, yaani, watu hawa wote waliosalia; maana tumesalia wachache tu katika watu wengi, kama macho yako yatuonavyo;
3. ili kwamba Bwana, Mungu wako, atuonyeshe njia ambayo yatupasa tuiendee, na jambo litupasalo tulitende.
4. Ndipo Yeremia, nabii, akawaambia, Nimewasikia; tazama, nitamwomba Bwana, Mungu wenu, sawasawa na maneno yenu; tena itakuwa, neno lo lote ambalo Bwana atawajibu, nitawaambia; sitawazuilia neno liwalo lote.
5. Wakamwambia Yeremia, Bwana na awe shahidi wa kweli na uaminifu kati yetu; ikiwa hatufanyi sawasawa na neno lile, ambalo Bwana, Mungu wako, atakutuma utuletee.
6. Likiwa jema, au likiwa baya, sisi tutaitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, ambaye tunakutuma kwake; ipate kuwa faida yetu, tunapoitii sauti ya Bwana, Mungu wetu.
7. Ikawa, baada ya siku kumi, neno la Bwana likamjia Yeremia.
8. Ndipo akamwita Yohana, mwana wa Karea, na maakida wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, na watu wote tangu wadogo hata wakubwa,
9. akawaambia, Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye mlinituma kwake, ili niyaweke maombi yenu mbele yake, asema hivi;
10. Ikiwa mtakaa bado katika nchi hii, ndipo nitawajenga, wala sitawabomoa, nami nitawapanda, wala sitawang'oa; kwa maana nayajutia mabaya niliyowatenda.
11. Msimwogope mfalme wa Babeli, mnayemwogopa; msimwogope, asema Bwana; maana mimi ni pamoja nanyi, niwaokoe, na kuwaponya na mkono wake.
12. Nami nitawapa rehema, kwamba awarehemu ninyi, na kuwarudisha mkae katika nchi yenu wenyewe.
13. Lakini mkisema, Hatutaki kukaa katika nchi hii; msiitii sauti ya Bwana, Mungu wenu;
14. mkisema, La! Lakini tutakwenda nchi ya Misri, ambayo hatutaona vita, wala kuisikia sauti ya tarumbeta, wala kuona njaa kwa kukosa chakula; nasi tutakaa huko;
15. basi, lisikieni neno la Bwana, enyi mabaki ya Yuda; Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ikiwa mwakaza nyuso zenu kuingia Misri, na kwenda kukaa huko;
16. basi, itakuwa, upanga mnaouogopa utawapata huko, katika nchi ya Misri, nayo njaa mnayoiogopa itawafuatia mbio huko Misri, nanyi mtakufa huko.
17. Haya ndiyo yatakayowapata watu wote waelekezao nyuso zao kwenda Misri, na kukaa huko; watakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni; hapana mtu awaye yote miongoni mwao atakayesalia, au kuokoka katika mabaya nitakayoyaleta juu yao.
18. Maana Bwana wa majeshi Mungu wa Israeli, asema hivi, Kama hasira yangu, na ghadhabu yangu, ilivyomwagwa juu ya hao wakaao Yerusalemu, ndivyo ghadhabu yangu itakavyomwagwa juu yenu, mtakapoingia Misri; nanyi mtakuwa apizo, na ajabu, na laana, na aibu; wala hamtapaona mahali hapa tena.
19. Bwana asema katika habari zenu, enyi mabaki ya Yuda, Msiingie Misri; jueni sana ya kuwa nimewashuhudia hivi leo.
20. Maana mmetenda kwa hila juu ya nafsi zenu wenyewe; kwa kuwa mmenituma kwa Bwana, Mungu wenu, mkisema, Utuombee kwa Bwana, Mungu wetu, ukatufunulie sawasawa na yote atakayoyanena Bwana, Mungu wetu, nasi tutayatenda;
21. nami nimewafunulia haya leo; lakini ninyi hamkuitii sauti ya Bwana, Mungu wenu, katika neno lo lote ambalo amenituma kwenu.
22. Basi, sasa jueni sana ya kuwa mtakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, katika mahali pale mnapopatamani kwenda na kukaa.

  Jeremiah (42/52)