← Jeremiah (37/52) → |
1. | Na Sedekia, mwana wa Yosia, akamiliki badala ya Konia, mwana wa Yehoyakimu, ambaye Nebukadreza amemmilikisha katika nchi ya Yuda. |
2. | Lakini yeye, wala watumishi wake, wala watu wa nchi, hawakuyasikiliza maneno ya Bwana aliyonena kwa kinywa cha nabii Yeremia. |
3. | Sedekia, mfalme, akamtuma Yehukali, mwana wa Shelemia, na Sefania, mwana wa Maaseya, kuhani, kwa Yeremia, nabii, kusema, Utuombee sasa kwa Bwana, Mungu wetu. |
4. | Basi Yeremia alikuwa akiingia na kutoka kati ya watu; kwa maana walikuwa hawakumfunga gerezani. |
5. | Na jeshi la Farao lilikuwa limetoka nchi ya Misri; na Wakaldayo waliohusuru Yerusalemu, waliposikia habari zao, wakavunja kambi yao mbele ya Yerusalemu. |
6. | Ndipo neno la Bwana likamjia nabii Yeremia, kusema, |
7. | Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mtamwambia hivi mfalme wa Yuda, aliyewatuma kwangu kuniuliza; Angalieni, jeshi la Farao, ambalo linakuja kuwasaidia, litarudi Misri, nchi yao wenyewe. |
8. | Na Wakaldayo watakuja tena, na kupigana na mji huu; nao watautwaa, na kuuteketeza. |
9. | Bwana asema hivi, Msijidanganye mkisema, Bila shaka Wakaldayo watatuacha na kwenda zao; maana hawatawaacha. |
10. | Maana mngelipiga jeshi lote la Wakaldayo wanaopigana nanyi, wakabaki kati yao watu waliojeruhiwa tu, hata hivyo wangeondoka kila mtu katika hema yake, na kuuteketeza mji huu. |
11. | Hata ikawa, jeshi la Wakaldayo lilipokuwa limevunja kambi yao mbele ya Yerusalemu, kwa kuliogopa jeshi la Farao, |
12. | ndipo Yeremia akatoka Yerusalemu, ili aende mpaka nchi ya Benyamini, alipokee huko fungu lake kati ya watu. |
13. | Naye alipokuwa katika lango la Benyamini, akida wa walinzi alikuwapo, jina lake Iriya, mwana wa Shelemia, mwana wa Hanania; akamkamata Yeremia, nabii, akisema, Unakwenda kujiunga na Wakaldayo. |
14. | Ndipo Yeremia akasema, Ni uongo, siendi kujiunga na Wakaldayo; lakini yeye asimsadiki; basi Iriya akamkamata Yeremia, akamleta kwa wakuu. |
15. | Nao wakuu wakamkasirikia Yeremia, wakampiga, wakamtia gerezani katika nyumba ya Yonathani, mwandishi; kwa maana ndiyo waliyoifanya kuwa gereza. |
16. | Basi, Yeremia alipokuwa ameingia katika nyumba ya shimo, na katika vyumba vya ndani; na Yeremia alipokuwa amekaa humo siku nyingi; |
17. | ndipo Sedekia, mfalme, akatuma watu wamlete; naye mfalme akamwuliza kwa siri ndani ya nyumba yake, akasema, Je! Liko neno lililotoka kwa Bwana? Yeremia akasema, Liko. Akasema pia, Utatiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli. |
18. | Pamoja na haya Yeremia akamwambia mfalme Sedekia, Nimefanya kosa gani juu yako, au juu ya watumishi wako, au juu ya watu hawa, hata mkanitia gerezani? |
19. | Wako wapi sasa manabii wenu waliowatabiria, wakisema, Mfalme wa Babeli hatakuja juu yenu, wala juu ya nchi hii? |
20. | Na sasa unisikilize, Ee bwana wangu mfalme; maombi yangu yakapate kibali mbele yako; usinirudishe nyumbani mwa Yonathani, mwandishi, nisije nikafa humo. |
21. | Ndipo Sedekia mfalme akatoa amri, wakamtia Yeremia katika uwanda wa walinzi; wakampa kila siku mkate mmoja uliotoka katika njia ya waokaji, hata mkate wote wa mji ulipokwisha. Basi Yeremia akakaa katika uwanda wa walinzi. |
← Jeremiah (37/52) → |