Jeremiah (33/52)  

1. Tena, neno la Bwana likamjia Yeremia mara ya pili, hapo alipokuwa akali amefungwa katika uwanda wa walinzi, kusema,
2. Bwana alitendaye jambo hili, Bwana aliumbaye ili alithibitishe; Bwana ndilo jina lake; asema hivi,
3. Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.
4. Maana Bwana, Mungu wa Israeli asema hivi, katika habari za nyumba za mji huu, na katika habari za nyumba za wafalme wa Yuda, zilizobomolewa ili kuyapinga maboma na upanga;
5. Wanakuja kupigana na Wakaldayo, lakini ni kuzijaza kwa mizoga ya watu, niliowaua katika hasira yangu na ghadhabu yangu, ambao kwa ajili ya uovu wao wote nimeuficha mji huu uso wangu.
6. Tazama, nitauletea afya na kupona, nami nitawaponya; nami nitawafunulia wingi wa amani na kweli.
7. Nami nitawarudisha wafungwa wa Yuda, na wafungwa wa Israeli, na kuwajenga kama kwanza.
8. Nami nitawasafisha na uovu wao wote, ambao kwa huo wamenitenda dhambi; nami nitawasamehe maovu yao yote, ambayo kwayo wamenitenda dhambi, na kukosa juu yangu.
9. Na mji huu utakuwa kwangu jina la furaha, na sifa na utukufu, mbele ya mataifa yote ya dunia, watakaosikia habari ya mema yote niwatendeayo, nao wataogopa na kutetemeka, kwa sababu ya mema yote na amani nitakaoupatia mji huo.
10. Bwana asema hivi, katika mahali hapo ambapo mnasema kwamba ni ukiwa, hapana mwanadamu wala mnyama, naam, katika miji ya Yuda na katika njia za Yerusalemu, zilizo ukiwa, hazina mwanadamu wala mwenyeji wala mnyama,
11. itasikilikana tena sauti ya furaha na sauti ya shangwe, sauti ya bwana arusi na sauti ya bibi arusi, sauti yao wasemao Mshukuruni Bwana wa majeshi, maana Bwana ni mwema, rehema zake ni za milele; na sauti zao waletao sadaka za shukrani nyumbani kwa Bwana. Kwa kuwa nitawarudisha wafungwa wa nchi hii kama kwanza, asema Bwana.
12. Bwana wa majeshi asema hivi, Katika mahali hapa, palipo ukiwa, hapana mwanadamu wala mnyama, na katika miji yake yote, yatakuwapo makao ya wachungaji wakizilaza kondoo zao.
13. Katika miji ya nchi ya vilima, katika miji ya nchi tambarare, katika miji ya Negebu, na katika nchi ya Benyamini, na katika mahali palipo karibu na Yerusalemu, na katika miji ya Yuda, makundi ya kondoo yatapita tena chini ya mikono yake awahesabuye, asema Bwana.
14. Tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapolitimiza neno lile jema nililolinena, katika habari za nyumba ya Israeli, na katika habari za nyumba ya Yuda.
15. Katika siku zile, na wakati ule, nitamchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atafanya hukumu na haki katika nchi hii.
16. Katika siku zile Yuda ataokolewa, na Yerusalemu utakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu.
17. Maana Bwana asema hivi, Daudi hatakosa kuwa na mtu wa kuketi katika kiti cha enzi cha nyumba ya Israeli;
18. wala makuhani Walawi hawatakosa kuwa na mtu wa kusimama mbele zangu, na kutoa sadaka za kuteketezwa, na kufukiza matoleo, na kufanya dhabihu daima.
19. Neno la Bwana likamjia Yeremia, kusema,
20. Bwana asema hivi, Kama mkiweza kulivunja agano langu la mchana, na agano langu la usiku, hata usiwepo tena mchana na usiku kwa wakati wake,
21. ndipo agano langu nililolifanya na Daudi, mtumishi wangu, laweza kuvunjika, hata asiwe na mwana wa kumiliki katika kiti chake cha enzi; tena agano langu nililofanya na Walawi makuhani, wahudumu wangu, laweza kuvunjika.
22. Kama vile jeshi la mbinguni haliwezi kuhesabiwa, wala mchanga wa bahari kupimwa; ndivyo nitakavyoongeza wazao wa Daudi, mtumishi wangu, na Walawi wanaonihudumia.
23. Kisha neno la Bwana likamjia Yeremia, kusema,
24. Je! Hufikiri neno hili walilolisema watu hawa, wakinena, Jamaa zile mbili alizozichagua Bwana amezitupilia mbali? Hivyo ndivyo wanavyowadharau watu wangu, ili wasiwe taifa tena mbele yao.
25. Bwana asema hivi, Ikiwa agano langu la mchana na usiku halikai imara, ikiwa mimi sikuziamuru kawaida za mbingu na dunia;
26. ndipo nitawatupilia mbali wazao wa Yakobo, na Daudi, mtumishi wangu, hata nisitwae wazao wake watawale juu ya wazao wa Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; kwa maana nitawarudisha wafungwa wao, nami nitawarehemu.

  Jeremiah (33/52)