Jeremiah (28/52)  

1. Ikawa, katika mwaka ule ule, mwanzo wa kutawala kwake Sedekia, mfalme wa Yuda, mwaka wa nne, mwezi wa tano, Hanania, mwana wa Azuri, nabii, wa Gibeoni, akasema nami ndani ya nyumba ya Bwana, mbele ya makuhani na watu wote, akisema,
2. Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nimeivunja nira ya mfalme wa Babeli.
3. Kabla haujatimia muda wa miaka miwili mizima, nitavirudisha mahali hapa vyombo vyote vya nyumba ya Bwana, ambavyo Nebukadreza, mfalme wa Babeli, aliviondoa katika mahali hapa, akavichukua mpaka Babeli.
4. Nami nitamrudisha hapa Yekonia, mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, pamoja na mateka wote wa Yuda, waliokwenda Babeli, asema Bwana; maana nitaivunja nira ya mfalme wa Babeli.
5. Ndipo nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, mbele ya makuhani, na mbele ya watu wote waliosimama ndani ya nyumba ya Bwana,
6. naam, nabii Yeremia akasema, Amina, Bwana na atende hivi; Bwana ayatimize maneno yako uliyotabiri, kuvirudisha hapa vyombo vya nyumba ya Bwana na watu wote waliofungwa, toka Babeli, hata mahali hapa.
7. Lakini lisikilize sasa neno hili nilisemalo, masikioni mwako, na masikioni mwa watu wote,
8. Manabii waliokuwako kabla ya zamani zangu, na zamani zako, walitabiri juu ya nchi nyingi, na juu ya falme kubwa, habari ya vita, na ya mabaya, na ya tauni.
9. Nabii atabiriye habari za amani, neno la nabii yule litakapotokea, ndipo nabii yule atakapojulikana, kuwa Bwana amemtuma kweli kweli.
10. Ndipo nabii Hanania akaitwaa hiyo nira iliyokuwa juu ya shingo ya Yeremia, akaivunja.
11. Naye Hanania akanena mbele ya watu wote, akisema, Bwana asema hivi, Hivyo ndivyo nitakavyoivunja nira ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, kabla haujatimia muda wa miaka miwili mizima, na kuiondoa shingoni mwa mataifa yote. Basi nabii Yeremia akaenda zake.
12. Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia, baada ya Hanania, nabii, kuivunja ile nira iliyokuwa juu ya shingo ya Yeremia, kusema,
13. Enenda ukamwambie Hanania, ukisema, Bwana asema hivi, Umezivunja nira za mti; lakini badala yake utafanya nira za chuma.
14. Maana Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nimetia nira ya chuma juu ya shingo ya mataifa haya yote, ili wamtumikie Nebukadreza, mfalme wa Babeli nao watamtumikia; nami nimempa wanyama wa nchi pia.
15. Kisha nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, Sikia sasa, Ee Hanania; Bwana hakukutuma; lakini unawatumainisha watu hawa maneno ya uongo.
16. Basi Bwana asema hivi, Tazama, nakutuma uende zako toka juu ya uso wa nchi; mwaka huu utakufa, kwa sababu umenena maneno ya uasi juu ya Bwana.
17. Basi nabii Hanania akafa, mwaka uo huo, mwezi wa saba.

  Jeremiah (28/52)