Jeremiah (26/52)  

1. Mwanzo wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili lilitoka kwa Bwana, kusema,
2. Bwana asema hivi, Simama katika uwanja wa nyumba ya Bwana, useme na miji yote ya Yuda, wajao ili kuabudu katika nyumba ya Bwana; sema nao maneno yote ninayokuamuru kuwaambia, usizuie hata neno moja.
3. Labda watasikia, na kughairi na kuacha kila mtu njia yake mbaya; ili niyaghairi mabaya niliyokusudia kuwatenda, kwa sababu ya uovu wa matendo yao.
4. Nawe utawaambia, Bwana asema hivi, Kama hamtaki kunisikia, kwenda katika sheria yangu, niliyoiweka mbele yenu,
5. kuyasikiliza maneno ya watumishi wangu, manabii, ninaowatuma kwenu, naam, nikiondoka mapema na kuwatuma; lakini ninyi hamkuwasikiliza;
6. basi, nitafanya nyumba hii kuwa kama Shilo, na mji huu nitaufanya kuwa laana kwa taifa zote za dunia.
7. Na makuhani, na manabii, na watu wote, wakamsikia Yeremia, hapo aliposema maneno haya katika nyumba ya Bwana.
8. Ikawa, Yeremia alipokuwa amekwisha kusema maneno yote Bwana aliyomwamuru kuwaambia watu wote, ndipo hao makuhani, na manabii, na watu wote, wakamkamata, wakisema, Bila shaka utakufa.
9. Kwa nini umetabiri kwa jina la Bwana, ukisema, Nyumba hii itakuwa kama Shilo, na mji huu utakuwa ukiwa, hautakaliwa na mtu? Watu wote wakamkusanyikia Yeremia katika nyumba ya Bwana.
10. Na wakuu wa Yuda waliposikia habari za mambo haya, wakatoka katika nyumba ya mfalme, wakapanda juu mpaka nyumbani kwa Bwana; wakaketi, hapo watu waingiapo katika lango jipya la nyumba ya Bwana.
11. Ndipo hapo makuhani, na manabii, wakawaambia wakuu na watu wote, wakisema, Mtu huyu amestahili kufa, kwa sababu ametabiri juu ya mji huu, kama mlivyosikia kwa masikio yenu.
12. Ndipo Yeremia akawaambia wakuu wote na watu wote, akisema, Bwana ndiye aliyenituma kutabiri juu ya nyumba hii, na juu ya mji huu, maneno hayo yote mliyoyasikia.
13. Basi sasa, tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, mkaisikilize sauti ya Bwana, Mungu wenu; naye Bwana atayaghairi mabaya aliyoyanena juu yenu.
14. Lakini kwangu mimi, tazama, mimi nipo hapa mikononi mwenu; nitendeni myaonayo kuwa mema na haki mbele ya macho yenu.
15. Lakini jueni yakini ya kuwa, mkiniua, mtajiletea juu yenu damu isiyo na hatia itakuwa juu yenu, na juu ya mji huu, na juu ya wenyeji wake; kwa maana ni kweli Bwana amenituma kwenu, kuwaambieni yote mliyoyasikia.
16. Ndipo wakuu na watu wote wakawaambia makuhani, na manabii, wakisema, Mtu huyu hastahili kuuawa; kwa maana amesema nasi katika jina la Bwana Mungu wetu.
17. Ndipo watu kadha wa kadha miongoni mwa wazee wa nchi wakaondoka, wakanena na mkutano wa watu, wakisema,
18. Mikaya Mmorashti, alitabiri katika siku za Hezekia, mfalme wa Yuda; akasema na watu wote wa Yuda, ya kwamba, Bwana wa majeshi asema hivi, Sayuni utalimwa kama shamba lilimwavyo, na Yerusalemu utakuwa magofu, na mlima wa nyumba utakuwa kama mahali palipoinuka msituni.
19. Je! Hezekia, mfalme wa Yuda, na watu wote wa Yuda, walimwua Mikaya? Je! Hakumcha Bwana, na kumwomba Bwana awafadhili; naye Bwana akaghairi, asiyatende mabaya yale aliyoyatamka juu yao? Na sisi tungetenda mabaya makuu juu ya roho zetu.
20. Tena, kulikuwa na mtu aliyetabiri katika jina la Bwana, Uria, mwana wa Shemaya, wa Kiriath-Yearimu; yeye naye alitabiri juu ya mji huu, na juu ya nchi hii, sawasawa na maneno yote ya Yeremia;
21. na Yehoyakimu, mfalme, na mashujaa wake wote, na wakuu wake wote, waliposikia maneno yake, mfalme akataka kumwua; lakini Uria alipopata habari, aliogopa, akakimbia akaenda Misri.
22. Basi, mfalme Yehoyakimu akatuma watu waende Misri, Elnathani, mwana wa Akbori, na watu wengine pamoja naye, kwenda Misri;
23. wakamtoa Uria katika Misri, wakamleta kwa Yehoyakimu, mfalme; naye akamwua kwa upanga, akamtupa yule maiti katika makaburi ya watu wasio na cheo.
24. Lakini mkono wa Ahikamu, mwana wa Shafani, alikuwa pamoja na Yeremia, wasimtie katika mikono ya watu auawe.

  Jeremiah (26/52)