| ← Jeremiah (2/52) → |
| 1. | Neno la Bwana likanijia, kusema, |
| 2. | Enenda ukalie masikioni mwa Yerusalemu, ukisema, Bwana asema hivi, Nakukumbuka, hisani ya ujana wako, upendo wa wakati wa uposo wako; Jinsi ulivyonifuata huko jangwani, katika nchi isiyopandwa mbegu. |
| 3. | Israeli walikuwa utakatifu kwa Bwana; malimbuko ya uzao wake; Wote watakaomla watakuwa na hatia; uovu utawajilia; asema Bwana. |
| 4. | Lisikieni neno la Bwana, ninyi nyumba ya Yakobo, na ninyi, jamaa zote za nyumba ya Israeli. |
| 5. | Bwana asema hivi, Baba zenu waliona dhuluma gani kwangu, hata wakafarakana nami, wakafuata ubatili, nao wakawa ubatili? |
| 6. | Wala hawakusema, Yuko wapi Bwana, aliyetutoa katika nchi ya Misri; akatuongoza jangwani, katika nchi ya ukame na mashimo, katika nchi ya kiu na ya kivuli cha mauti, katika nchi ambayo ndani yake hapiti mtu, wala haikukaliwa na watu? |
| 7. | Nami nikawatia katika nchi ya shibe, mpate kula matunda yake na mema yake; lakini ninyi mlipoingia katika nchi ile, mliitia unajisi nchi yangu, na urithi wangu mliufanya kuwa chukizo. |
| 8. | Makuhani hawakusema, Yuko wapi Bwana? Wala wana-sheria hawakunijua; wachungaji nao waliniasi, nao manabii walitoa unabii kwa Baali, wakafuata mambo yasiyofaidia kitu. |
| 9. | Basi, kwa ajili ya hayo nitateta nanyi, asema Bwana, nami nitateta na watoto wa watoto wenu. |
| 10. | Maana, vukeni mpaka visiwa vya Kitimu, mkaone; tumeni watu waende Kedari, mkafikiri sana; mkaone kwamba jambo kama hili limekuwa wakati wo wote. |
| 11. | Je! Taifa wamebadili miungu yao, ingawa siyo miungu? Lakini watu wangu wameubadili utukufu wao kwa ajili ya kitu kisichofaidia. |
| 12. | Enyi mbingu, staajabuni kwa ajili ya jambo hili, mkaogope sana, na kuwa ukiwa sana, asema Bwana. |
| 13. | Kwa maana watu wangu hawa wametenda maovu mawili; wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji ya uzima, wamejichimbia mabirika, mabirika yavujayo, yasiyoweza kuweka maji. |
| 14. | Je! Israeli ni mtumwa? Je! Ni mzalia? mbona amekuwa mateka? |
| 15. | Wana-simba wamenguruma juu yake, wametoa sana sauti zao; Nao wameifanya nchi yake kuwa ukiwa; miji yake imeteketea, haina watu. |
| 16. | Tena wana wa Nofu na Tahpanesi wamevunja utosi wa kichwa chako. |
| 17. | Je! Hukujipatia mambo haya mwenyewe, kwa kuwa umemwacha Bwana, Mungu wako, alipokuongoza njiani? |
| 18. | Na sasa una nini utakayotenda katika njia iendayo Misri, kunywa maji ya Shihori? Au una nini utakayotenda katika njia iendayo Ashuru, kunywa maji ya ule Mto? |
| 19. | Uovu wako mwenyewe utakurudi, maasi yako yatakukaripia; ujue, basi, ukaone, ya kuwa ni jambo baya sana na uchungu, kuwa umemwacha Bwana, Mungu wako, na ya kuwa moyoni mwako hamna kunihofu, asema Bwana, Bwana wa majeshi. |
| 20. | Kwa maana tangu zamani wewe umeivunja nira yako, na kuvipasua vifungo vyako; ukasema, Mimi sitatumika; kwa maana juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi, umejiinamisha, ukafanya mambo ya ukahaba. |
| 21. | Nami nalikuwa nimekupanda, mzabibu mwema sana, mbegu nzuri kabisa; umegeukaje, basi, kuwa mche usiofaa wa mzabibu-mwitu machoni pangu? |
| 22. | Maana ujapojiosha kwa magadi, na kujipatia sabuni nyingi, lakini uovu wako umeandikwa mbele zangu, asema Bwana MUNGU. |
| 23. | Wawezaje kusema, Sikutiwa unajisi, sikuwafuata Mabaali? Itazame njia yako bondeni, ujue uliyoyatenda; wewe u ngamia mwepesi, apitaye katika njia zake; |
| 24. | punda wa mwitu aliyeizoelea nyika, avutaye pumzi za upepo katika tamaa yake; katika wakati wake ni nani awezaye kumgeuza? Wote wamtafutao hawatajichokesha nafsi zao; katika mwezi wake watamwona. |
| 25. | Zuia mguu wako usikose kiatu, na koo yako isiwe na kiu; lakini wewe ulisema, Hapana matumaini kabisa; la, maana nimewapenda wageni, nami nitawafuata. |
| 26. | Kama mwivi aonavyo haya akamatwapo, ndivyo waonavyo haya nyumba ya Israeli; wao, na wafalme wao, na wakuu wao, na makuhani wao, na manabii wao; |
| 27. | waliambiao gogo la mti, Wewe u baba yangu; na kuliambia jiwe, Ndiwe uliyenizaa; kwa maana wamenipa mimi visogo, wala hawakunielekezea nyuso zao; lakini wakati wa taabu watasema, Simama ukatuokoe. |
| 28. | Lakini wako wapi miungu yako ulioifanya? Na wasimame hao, kama wakiweza kukuokoa wakati wa taabu yako; kwa maana hesabu ya miungu yako ni sawasawa na hesabu ya miji yako, Ee Yuda. |
| 29. | Mbona mnataka kuteta nami? Ninyi nyote mmeniasi, asema Bwana. |
| 30. | Nimewapiga watoto wako bure; hawakukubali kurudiwa; upanga wenu wenyewe umewala manabii wako, kama simba aharibuye. |
| 31. | Ee kizazi litazameni neno la Bwana. Je! Nimekuwa jangwa kwa Israeli? Au nchi yenye giza kuu? Mbona watu wangu wanasema, Sisi tumetoroka, hatutaki kuja kwako tena? |
| 32. | Je! Mwanamwali aweza kusahau mapambo yake, au bibi arusi mavazi yake? Lakini watu wangu wamenisahau mimi kwa muda wa siku zisizo na hesabu. |
| 33. | Jinsi ulivyoitengeneza njia yako ili kutafuta mapenzi! Kwa sababu hiyo hata wanawake wabaya umewafundisha njia zako. |
| 34. | Tena katika pindo za nguo zako imeonekana damu ya roho zao maskini wasio na hatia; sikuiona penye mahali palipobomoka, lakini naliiona juu ya hawa wote. |
| 35. | Lakini ulisema, Sina hatia mimi; bila shaka hasira yake imegeuka na kuniacha. Tazama, nitaingia hukumuni pamoja nawe, kwa sababu unasema, Sikutenda dhambi mimi. |
| 36. | Mbona unatanga-tanga hivi upate kugeuza mwendo wako? Utaona haya kwa ajili ya Misri pia, kama ulivyoona haya kwa ajili ya Ashuru. |
| 37. | Hata kwake pia utatoka, na mikono yako juu ya kichwa chako; kwa maana Bwana amewakataa uliowakimbilia, wala hutafanikiwa katika hao. |
| ← Jeremiah (2/52) → |