Jeremiah (19/52)  

1. Bwana akasema hivi, Enenda ukanunue gudulia la mfinyanzi, ukachukue pamoja nawe baadhi ya wazee wa watu, na baadhi ya wazee wa makuhani;
2. ukatoke uende mpaka bonde la mwana wa Hinomu lililo karibu na mahali pa kuingia kwa lango la vigae, ukahubiri huko maneno nitakayokuambia,
3. ukisema, Lisikieni neno la Bwana, enyi wafalme wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu; Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli asema hivi, Angalieni, nitaleta mabaya juu ya mahali hapa, ambayo mtu ye yote akisikia habari yake, masikio yake yatawaka.
4. Kwa sababu wameniacha mimi, nao wamepafanya mahali hapa kuwa mahali pageni, nao hapa wamewafukizia uvumba miungu mingine wasiowajua, wala wao, wala baba zao, wala wafalme wa Yuda; nao wamepajaza mahali hapa damu ya wasio na hatia;
5. nao wamemjengea Baali mahali pake palipo juu, ili kuwachoma moto wana wao, wawe sadaka za kuteketezwa kwa Baali; tendo nisiloliamuru mimi, wala kulinena, wala halikuingia moyoni mwangu;
6. basi, angalieni, siku zinakuja, asema Bwana, ambazo katika siku hizo mahali hapa hapataitwa tena Tofethi, wala Bonde la mwana wa Hinomu, bali, Bonde la Machinjo.
7. Nami nitalitangua shauri la Yuda na Yerusalemu mahali hapa; nami nitawaangusha kwa upanga mbele za adui zao, na kwa mkono wa watu watafutao roho zao; na mizoga yao nitawapa ndege wa angani na wanyama wakali wa nchi, iwe chakula chao.
8. Nami nitaufanya mji huu kuwa kitu cha kushangaza watu, na kuzomewa; kila mtu apitaye karibu nao atashangaa, na kuzomea kwa sababu ya mapigo yake.
9. Nami nitawalazimisha kula nyama ya wana wao, na nyama ya binti zao, nao watakula kila mmoja nyama ya rafiki yake, wakati wa mazingira na dhiki, ambayo adui zao, na watu wale watafutao roho zao, watawadhiikisha.
10. Ndipo hapo utalivunja gudulia lile, mbele ya macho ya watu wale waendao pamoja nawe,
11. na kuwaambia, Bwana wa majeshi asema hivi, Hivyo ndivyo nitakavyowavunja watu hawa, na mji huu, kama mtu avunjavyo chombo cha mfinyanzi, kisichoweza kutengenezwa tena na kuwa kizima; nao watazika watu katika Tofethi hata hapatabaki mahali pa kuzika.
12. Hivyo ndivyo nitakavyopatenda mahali hapa, asema Bwana, nao wakaao humo, hata kufanya mji huu kuwa kama Tofethi;
13. na nyumba za Yerusalemu, na nyumba za wafalme wa Yuda, zilizotiwa unajisi, zitakuwa kama mahali pa Tofethi; naam, nyumba zote ambazo juu ya dari zake wamelifukizia uvumba jeshi lote la mbinguni, na kuwamiminia miungu mingine sadaka za kunywewa.
14. Kisha Yeremia akatoka huko Tofethi, huko ambako Bwana alimtuma atoe unabii; naye akasimama katika ua wa nyumba ya Bwana, akawaambia watu wote,
15. Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitaleta juu ya mji huu, na juu ya vijiji vyake vyote, mabaya yote niliyoyanena juu yake; kwa sababu wamefanya shingo zao kuwa ngumu, kusudi wasiyasikie maneno yangu.

  Jeremiah (19/52)