Jeremiah (15/52)  

1. Ndipo Bwana akaniambia, Hata wangesimama mbele zangu Musa na Samweli, moyo wangu usingewaelekea watu hawa; watupe, watoke mbele za macho yangu, wakaende zao.
2. Kisha itakuwa, hapo watakapokuambia, Tutoke, tuende wapi? Utawaambia, Bwana asema hivi, Walioandikiwa kufa, watakwenda kufa; au kufa kwa upanga, watakufa kwa upanga; au kufa kwa njaa, watakufa kwa njaa, au kutekwa nyara, watakuwa mateka.
3. Nami nitaamrisha juu yao namna nne, asema Bwana; upanga uue, na mbwa wararue, na ndege wa angani, na wanyama wakali wa nchi, wale na kuangamiza.
4. Nami nitawafanya kuwa kitu cha kutisha katika falme zote za duniani, kwa sababu ya Manase, mwana wa Hezekia mfalme wa Yuda, kwa sababu ya mambo aliyoyatenda katika Yerusalemu.
5. Maana ni nani atakayekuhurumia, Ee Yerusalemu? Au ni nani atakayekulilia? Au ni nani atakayegeuka upande ili kuuliza habari za hali yako?
6. Umenikataa mimi, asema Bwana, umerudi nyuma; ndiyo maana nimenyosha mkono wangu juu yako, na kukuangamiza; nimechoka kwa kughairi.
7. Nami nimewapepea kwa kipepeo katika malango ya nchi nimewaondolea watoto wao, nimewaharibu watu wangu; hata hivyo hawakurudi na kuziacha njia zao.
8. Wajane wao wameongezeka kwangu kuliko mchanga wa bahari; nimeleta mwenye kuteka wakati wa adhuhuri juu ya mama wa vijana; nimeleta hamu na maogofyo yampate ghafula.
9. Mwanamke aliyezaa watoto saba anazimia; ametoa roho; jua lake limekuchwa, ungali ni wakati wa mchana; ametahayarika na kufedheheka; na mabaki yao nitawatoa kwa upanga mbele ya adui zao, asema Bwana.
10. Ole wangu, mama yangu, kwa kuwa umenizaa mtu wa kuteta, na mtu wa kushindana na dunia yote! Mimi sikukopesha kwa riba, wala watu hawakunikopesha kwa riba; lakini kila mmoja wao hunilaani.
11. Bwana akasema, Hakika nitakutia nguvu upate mema; hakika nitamlazimisha adui akusihi wakati wa uovu, na wakati wa taabu.
12. Je! Mtu aweza kuvunja chuma, naam, chuma kitokacho kaskazini, au shaba?
13. Mali yako na hazina zako nitazitoa kuwa nyara, bila kulipwa thamani yake; naam, kwa sababu ya dhambi zako zote, hata katika mipaka yako yote.
14. Nami nitakulazimisha kuwatumikia adui zako katika nchi usiyoijua; maana moto umewashwa katika hasira yangu, utakaowateketeza ninyi.
15. Ee Bwana, unajua wewe; unikumbuke, unijilie, ukanilipie kisasi juu yao wanaoniudhi; usiniondoe kwa uvumilivu wako; ujue ya kuwa ni kwa ajili yako nilivyopatikana na mashutumu.
16. Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana, Mungu wa majeshi.
17. Sikuketi katika mkutano wao wanaojifurahisha, wala sikufurahi, naliketi peke yangu kwa sababu ya mkono wako; kwa maana umenijaza ghadhabu.
18. Mbona maumivu yangu ni ya daima, na jeraha yangu haina dawa, inakataa kuponywa? Je! Yamkini wewe utakuwa kwangu kama kijito kidanganyacho, na kama maji yasiyodumu?
19. Kwa sababu hiyo Bwana asema hivi, Ukirudi, ndipo mimi nitakapokurejeza, upate kusimama mbele zangu; nawe ukitoa kilicho cha thamani katika kilicho kibovu, utakuwa kama kinywa changu; nao watakurudia wewe, bali hutawarudia wao.
20. Nami nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya, asema Bwana.
21. Nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya, nami nitakukomboa katika mkono wao wenye kutisha.

  Jeremiah (15/52)