| ← Jeremiah (10/52) → | 
| 1. | Enyi nyumba ya Israeli, lisikieni neno awaambialo Bwana; | 
| 2. | Bwana asema hivi, Msijifunze njia ya mataifa, wala msishangae kwa sababu ya ishara za mbinguni; maana mataifa hushangaa kwa sababu ya ishara hizo. | 
| 3. | Maana desturi za watu hao ni ubatili, maana mtu mmoja hukata mti mwituni, kazi ya mikono ya fundi na shoka. | 
| 4. | Huupamba kwa fedha na dhahabu; huukaza kwa misumari na nyundo, usitikisike. | 
| 5. | Mfano wao ni mfano wa mtende, kazi ya cherehani, hawasemi; hawana budi kuchukuliwa, kwa sababu hawawezi kwenda. Usiwaogope; kwa maana hawawezi kutenda uovu, wala hawana uwezo wa kutenda mema. | 
| 6. | Hapana hata mmoja aliye kama wewe, Ee Bwana; wewe ndiwe uliye mkuu, na jina lako ni kuu katika uweza. | 
| 7. | Ni nani asiyekucha wewe, Ee mfalme wa mataifa? Maana hii ni sifa yako wewe; kwa kuwa miongoni mwa wenye hekima wote wa mataifa, na katika hali yao ya enzi yote pia, hapana hata mmoja kama wewe. | 
| 8. | Lakini wote pia huwa kama wanyama, ni wapumbavu. Haya ni maelezo ya sanamu, ni shina la mti tu. | 
| 9. | Iko fedha iliyofuliwa ikawa mabamba, iliyoletwa kutoka Tarshishi, na dhahabu kutoka Ufazi, kazi ya stadi na ya mikono ya mfua dhahabu; mavazi yao ni rangi ya samawi na urujuani; hayo yote ni kazi ya mafundi yao. | 
| 10. | Bali Bwana ndiye Mungu wa kweli; Ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele; Mbele za ghadhabu yake nchi yatetemeka, Wala mataifa hawawezi kustahimili hasira yake. | 
| 11. | Mtawaambia hivi, Miungu hiyo isiyofanya mbingu na nchi, hiyo itaangamia katika nchi, nayo itatoweka chini ya mbingu. | 
| 12. | Ameiumba dunia kwa uweza wake, Ameuthibitisha ulimwengu kwa hekima yake, Na kwa ufahamu wake amezitandika mbingu. | 
| 13. | Atoapo sauti yake, pana mshindo wa maji mbinguni, Naye hupandisha mawingu toka ncha za nchi; Huifanyia mvua umeme, Huutoa upepo katika hazina zake. | 
| 14. | Kila mtu amekuwa kama mnyama, hana maarifa; Kila mfua dhahabu amefedheheshwa na sanamu yake ya kuchonga; Maana sanamu yake ya kuyeyuka ni uongo, Wala hamna pumzi ndani yake. | 
| 15. | Ni ubatili tu, ni kazi za udanganyifu; Wakati wa kujiliwa kwao watapotea. | 
| 16. | Yeye, Fungu la Yakobo, siye kama hawa; Maana ndiye aliyeviumba vitu vyote; Na Israeli ni kabila ya urithi wake; Bwana wa majeshi ndilo jina lake. | 
| 17. | Haya! Kusanya bidhaa yako katika nchi, wewe ukaaye katika mazingiwa. | 
| 18. | Maana Bwana asema hivi, Tazama, wakati huu nitawatupa wenyeji wa nchi hii kama kwa kombeo, nitawataabisha, wapate kuona taabu. | 
| 19. | Ole wangu, kwa sababu ya jeraha yangu! Pigo langu laumia; lakini nalisema, Kweli, ni huzuni yangu mimi, nami sina budi kuivumilia. | 
| 20. | Hema yangu umetekwa nyara, kamba zangu zote zimekatika; watoto wangu wameniacha na kwenda zao, pia hawako. Hapana mtu atakayenitandikia tena hema yangu, na kuyatundika mapazia yangu. | 
| 21. | Kwa sababu wachungaji wamekuwa kama wanyama, wala hawakuuliza kwa Bwana; basi hawakufanikiwa, na makundi yao yote yametawanyika. | 
| 22. | Sauti imesikiwa, Tazama, inakuja; mshindo mkuu kutoka nchi ya kaskazini, ili kuifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa, makao ya mbweha. | 
| 23. | Ee Bwana, najua ya kuwa njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu. | 
| 24. | Ee Bwana, unirudi kwa haki; si kwa hasira yako, usije ukaniangamiza. | 
| 25. | Hasira yako uwamwagie mataifa wasiokujua, na jamaa zao wasioliitia jina lako; kwa maana wamemla Yakobo, naam, wamemla kabisa na kumwangamiza, na kuyafanya makao yake kuwa ukiwa. | 
| ← Jeremiah (10/52) → |