| Jeremiah (1/52) → | 
| 1. | Maneno ya Yeremia, mwana wa Hilkia, mmoja wa makuhani waliokuwa katika Anathothi, katika nchi ya Benyamini; | 
| 2. | ambaye neno la Bwana lilimjia katika siku za Yosia, mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda, katika mwaka wa kumi na tatu wa kumiliki kwake. | 
| 3. | Tena lilikuja siku za Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, hata mwisho wa mwaka wa kumi na mmoja wa Sedekia, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; hata wakati ulipochukuliwa mateka Yerusalemu, katika mwezi wa tano. | 
| 4. | Neno la Bwana lilinijia, kusema, | 
| 5. | Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. | 
| 6. | Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. | 
| 7. | Lakini Bwana akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. | 
| 8. | Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana. | 
| 9. | Ndipo Bwana akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; Bwana akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako; | 
| 10. | angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda. | 
| 11. | Tena neno la Bwana likanijia, kusema, Yeremia, waona nini? Nikasema, Naona ufito wa mlozi. | 
| 12. | Ndipo Bwana akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize. | 
| 13. | Neno la Bwana likanijia mara ya pili, kusema, Waona nini? Nikasema, Naona sufuria lenye maji yatokotayo, na mdomo wake unaelekea toka upande wa kaskazini. | 
| 14. | Ndipo Bwana akaniambia, Toka kaskazini mabaya yatatokea, na kuwapata watu wote wakaao katika nchi hii. | 
| 15. | Kwa kuwa, tazama, nitaziita jamaa zote za falme za kaskazini, asema Bwana; nao watakuja, na kuweka kila mtu kiti chake cha enzi mbele ya mahali pa kuingilia malango ya Yerusalemu, na kuzielekea kuta zake pande zote, na kuielekea miji yote ya Yuda. | 
| 16. | Nami nitatamka hukumu zangu juu yao kwa habari ya uovu wao wote; kwa kuwa wameniacha mimi, wakaifukizia uvumba miungu mingine, wakaziabudu kazi za mikono yao wenyewe. | 
| 17. | Haya basi, wewe jifunge viuno, ukaondoke ukawaambie maneno yote niliyokuamuru; usifadhaike kwa ajili yao, nisije nikakufadhaisha wewe mbele yao. | 
| 18. | Maana, tazama, nimekufanya leo kuwa mji wenye boma, na nguzo ya chuma, na kuta za shaba, juu ya nchi yote; juu ya wafalme wa Yuda, na juu ya wakuu wake, na juu ya makuhani wake, na juu ya watu wa nchi hii. | 
| 19. | Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema Bwana, ili nikuokoe. | 
| Jeremiah (1/52) → |