← James (3/5) → |
1. | Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi. |
2. | Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu. |
3. | Angalieni, twatia lijamu katika vinywa vya farasi, ili wamtii, hivi twageuza mwili wao wote. |
4. | Tena angalieni merikebu; ingawa ni kubwa kama nini, na kuchukuliwa na pepo kali, zageuzwa na usukani mdogo sana, ko kote anakoazimia kwenda nahodha. |
5. | Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana. |
6. | Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum. |
7. | Maana kila aina ya wanyama, na ya ndege, na ya vitambaavyo, na ya vitu vilivyomo baharini, vinafugika, navyo vimekwisha kufugwa na wanadamu. |
8. | Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti. |
9. | Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu. |
10. | Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo. |
11. | Je! Chemchemi katika jicho moja hutoa maji matamu na maji machungu? |
12. | Ndugu zangu, Je! Mtini waweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini? Kadhalika chemchemi haiwezi kutoa maji ya chumvi na maji matamu. |
13. | N'nani aliye na hekima na ufahamu kwenu? Na aonyeshe kazi zake kwa mwenendo wake mzuri, katika upole wa hekima. |
14. | Lakini, mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli. |
15. | Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani. |
16. | Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya. |
17. | Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki. |
18. | Na tunda la haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani. |
← James (3/5) → |