← James (2/5) → |
1. | Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu. |
2. | Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; |
3. | nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu, |
4. | je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu? |
5. | Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao? |
6. | Bali ninyi mmemvunjia heshima maskini. Je! Matajiri hawawaonei ninyi na kuwavuta mbele ya viti vya hukumu? |
7. | Hawalitukani jina lile zuri mliloitwa? |
8. | Lakini mkiitimiza ile sheria ya kifalme kama ilivyoandikwa, Mpende jirani yako kama nafsi yako, mwatenda vema. |
9. | Bali mkiwapendelea watu, mwafanya dhambi na kuhukumiwa na sheria kuwa wakosaji. |
10. | Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote. |
11. | Kwa maana yeye aliyesema, Usizini, pia alisema, Usiue. Basi ijapokuwa hukuzini, lakini umeua, umekuwa mvunja sheria. |
12. | Semeni ninyi, na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria ya uhuru. |
13. | Maana hukumu haina huruma kwake yeye asiyeona huruma. Huruma hujitukuza juu ya hukumu. |
14. | Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa? |
15. | Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, |
16. | na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? |
17. | Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake. |
18. | Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu. |
19. | Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka. |
20. | Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai? |
21. | Je! Baba yetu Ibrahimu hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipomtoa Isaka mwanawe juu ya madhabahu? |
22. | Waona kwamba imani ilitenda kazi pamoja na matendo yake, na ya kwamba imani ile ilikamilishwa kwa njia ya matendo yale. |
23. | Maandiko yale yakatimizwa yaliyonena, Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa ni haki; naye aliitwa rafiki wa Mungu. |
24. | Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake. |
25. | Vivyo hivyo na Rahabu, yule kahaba naye, je! Hakuhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo, hapo alipowakaribisha wajumbe, akawatoa nje kwa njia nyingine? |
26. | Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa, vivyo hivyo na imani pasipo matendo imekufa. |
← James (2/5) → |