| ← Isaiah (8/66) → |
| 1. | Bwana akaniambia, Ujipatie ubao mkubwa ukaandike juu yake kwa kalamu ya binadamu, Kwa Maher-shalal-hash-bazi; |
| 2. | nami nitajipatia mashahidi waaminifu ili kuandika habari, yaani, Uria, kuhani, na Zekaria, mwana wa Yeberekia. |
| 3. | Nami nikamwendea huyo nabii mke, naye akapata mimba, akazaa mtoto mwanamume. Kisha Bwana akaniambia, Mwite jina lake Maher-shalal-hash-bazi. |
| 4. | Kwa maana kabla mtoto huyo hajapata kujua kusema, Baba yangu, na Mama yangu, hazina za Dameski na mateka ya Samaria yatachukuliwa mbele ya mfalme wa Ashuru. |
| 5. | Kisha Bwana akasema nami mara ya pili, akaniambia, |
| 6. | Kwa sababu watu hawa wameyakataa maji ya Shiloa yapitayo polepole, na kufurahi kwa ajili ya Resini na huyo mwana wa Remalia, |
| 7. | basi sasa angalia; Bwana aleta juu yao maji ya huo Mto, yenye nguvu, mengi sana, nayo ni mfalme wa Ashuru na utukufu wake wote; naye atakuja, na kupita juu ya mifereji yake yote, atafurika juu ya kingo zake zote; |
| 8. | naye atapita, atapita kwa kasi na kuingia Yuda; atafurika na kupita katikati, atafika hata shingoni; na kule kuyanyosha mabawa yake kutaujaza upana wa nchi yako, Ee Imanueli. |
| 9. | Fanyeni ghasia, enyi kabila za watu, Nanyi mtavunjwa vipande vipande; Tegeni masikio, ninyi nyote wa nchi zilizo mbali; Jikazeni viuno, nanyi mtavunjwa vipande vipande; Jikazeni viuno, nanyi mtavunjwa vipande vipande. |
| 10. | Fanyeni shauri pamoja, nalo litabatilika; Semeni neno, lakini halitasimama; Kwa maana Mungu yu pamoja nasi. |
| 11. | Maana Bwana aliniambia hivi, kwa mkono hodari, akanifundisha nisiende katika njia ya watu hawa, akisema, |
| 12. | Msiseme, Ni fitina, katika habari za mambo yote ambayo watu hawa watasema, Ni fitina; msihofu kwa hofu yao, wala msiogope. |
| 13. | Bwana wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu. |
| 14. | Naye atakuwa ni mahali patakatifu; bali ni jiwe la kujikwaza na mwamba wa kujikwaa kwa nyumba za Israeli zote mbili, na mtego na tanzi kwa wenyeji wa Yerusalemu. |
| 15. | Na wengi watajikwaa juu yake, na kuanguka na kuvunjika, na kunaswa na kukamatwa. |
| 16. | Ufunge huo ushuhuda, ukaitie muhuri sheria kati ya wanafunzi wangu. |
| 17. | Nami nitamngojea Bwana, awafichaye uso wake nyumba ya Yakobo, nami nitamtazamia. |
| 18. | Angalieni, mimi na watoto hawa niliopewa na Bwana tu ishara na ajabu katika Israeli, zitokazo kwa Bwana wa majeshi, yeye akaaye katika mlima Sayuni. |
| 19. | Na wakati watakapokuambia, Tafuta habari kwa watu wenye pepo na kwa wachawi; waliao kama ndege na kunong'ona; je! Haiwapasi watu kutafuta habari kwa Mungu wao? Je! Waende kwa watu waliokufa kwa ajili ya watu walio hai? |
| 20. | Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi. |
| 21. | Nao watapita katikati yake, wamedhikika sana na kuwa na njaa; na itakuwa watakapoona njaa, watalalamika na kuapa kwa mfalme wao, na kwa Mungu wao, na kuelekeza nyuso zao juu; |
| 22. | nao wataiangalia nchi, na, tazama, shida na giza; hapana changamko kwa sababu ya dhiki; nao watafukuzwa na kuingia katika giza kubwa. |
| ← Isaiah (8/66) → |