← Isaiah (57/66) → |
1. | Mwenye haki hupotea, wala hakuna atiaye hayo moyoni; na watu watauwa huondolewa, wala hakuna afikiriye ya kuwa mwenye haki ameondolewa asipatikane na mabaya. |
2. | Yeye huingia katika amani; wao hustarehe katika vitanda vyao, kila mtu aendaye katika unyofu wake. |
3. | Lakini ninyi karibuni hapa, enyi wana wa mwanamke mchawi, uzao wa mzinzi na kahaba. |
4. | Mnafanya dhihaka yenu juu ya nani? Mmepanua vinywa vyenu, na kutoa ndimi zenu? Je, ninyi si wana wa uasi, uzao wa uongo; |
5. | ninyi mnaowasha tamaa zenu kati ya mialoni, chini ya kila mti wenye majani mabichi; ninyi mnaoua watoto mabondeni, chini ya mianya ya majabali? |
6. | Sehemu yako i katika makokoto ya bonde; hayo ndiyo kura yako; umeyamwagia hayo sadaka ya kinywaji, umeyatolea sadaka ya unga; je! Niwe radhi na mambo hayo? |
7. | Umeweka kitanda chako juu ya mlima mrefu ulioinuka sana; ukaenda huko ili kutoa dhabihu. |
8. | Na nyuma ya milango na miimo umeweka kumbukumbu lako; kwa maana umejifunua nafsi yako kwa ajili ya mwingine, si kwa ajili yangu, ukakwea juu; umekipanua kitanda chako, nawe umefanya maagano na hao; ulikipenda kitanda chao hapo ulipokiona. |
9. | Ulimwendea mfalme na mafuta ya marhamu, ukaongeza manukato yako, ukawatuma wajumbe wako waende mbali, ukajidhili sana hata kuzimu. |
10. | Ulikuwa umechoka kwa ajili ya urefu wa njia yako; lakini hukusema, Hapana matumaini; ulipata kuhuishwa nguvu zako; kwa sababu hiyo hukuugua. |
11. | Tena ni nani uliyemwogopa na kumhofu, hata ukasema uongo, wala hukunikumbuka mimi, wala kuweka hayo moyoni? Je! Mimi sikunyamaza tangu zamani, hata huniogopi? |
12. | Mimi nitatangaza haki yako, na matendo yako hayatakufaa. |
13. | Utakapolia, na wakuponye hao uliowakusanya; lakini upepo utawachukua; uvuvio tu utawachukulia mbali; lakini yeye anayenitumaini ataimiliki nchi, na kuurithi mlima wangu mtakatifu. |
14. | Naye atasema, Tutieni, tutieni, Itengenezeni njia, Kiondoeni kila kikwazacho Katika njia ya watu wangu. |
15. | Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu. |
16. | Kwa kuwa sitashindana na watu siku zote, wala sitakuwa na hasira siku zote; maana roho ingezimia mbele zangu, na hizo nafsi nilizozifanya. |
17. | Kwa sababu ya uovu wa kutamani kwake naliona hasira, nikampiga; nalificha uso wangu, nikaona ghadhabu; naye akaendelea kwa ukaidi, kuifuata njia ya moyo wake mwenyewe. |
18. | Nimeziona njia zake; nami nitamponya; nitamwongoza pia, nitamrudishia faraja zake, yeye na hao wanaomlilia. |
19. | Mimi nayaumba matunda ya midomo; Amani, amani, kwake yeye aliye mbali, na kwake yeye aliye karibu; asema Bwana; nami nitamponya. |
20. | Bali wabaya wanafanana na bahari iliyochafuka; maana haiwezi kutulia, na maji yake hutoa tope na takataka. |
21. | Hapana amani kwa wabaya; asema Mungu wangu. |
← Isaiah (57/66) → |