← Isaiah (56/66) → |
1. | Bwana asema hivi, Shikeni hukumu, mkatende haki; kwa maana wokovu wangu u karibu kuja, na haki yangu kufunuliwa. |
2. | Heri afanyaye haya, na mwanadamu ayashikaye sana; azishikaye sabato asizivunje, auzuiaye mkono wake usifanye uovu wo wote. |
3. | Wala mgeni, aambatanaye na Bwana, asiseme hivi, Hakika yake Bwana atanitenga na watu wake; wala towashi asiseme, Mimi ni mti mkavu. |
4. | Kwa maana Bwana awaambia hivi matowashi, wanaozishika sabato zangu, na kuyachagua mambo yanipendezayo, na kulishika sana agano langu; |
5. | Nitawapa hawa nyumbani mwangu, na ndani ya kuta zangu, kumbukumbu na jina, lililo jema kuliko kuwa na wana na binti; nitawapa jina lidumulo milele, lisilokatiliwa mbali. |
6. | Na wageni, walioandamana na Bwana ili wamhudumu, na kulipenda jina la Bwana, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; |
7. | Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote. |
8. | Bwana MUNGU, akusanyaye waliofukuzwa katika Israeli asema, Pamoja na hayo nitamkusanyia na wengine, zaidi ya hao walio wake waliokusanywa. |
9. | Enyi hayawani wote wa nyikani, njoni, Mle, enyi hayawani wote wa mwituni. |
10. | Walinzi wake ni vipofu, wote pia hawana maarifa; wote ni mbwa walio bubu, hawawezi kulia; huota ndoto, hulala, hupenda usingizi. |
11. | Naam, mbwa hao wana choyo sana, hawashibi kamwe; na hao ni wachungaji wasioweza kufahamu neno; wote pia wamegeuka upande, wazifuate njia zao wenyewe, kila mmoja kwa faida yake, toka pande zote. |
12. | Husema, Njoni, nitaleta divai, Na tunywe sana kileo; Na kesho itakuwa kama leo, Sikukuu kupita kiasi. |
← Isaiah (56/66) → |