← Isaiah (55/66) → |
1. | Haya, kila aonaye kiu, njoni majini, Naye asiye na fedha; njoni, nunueni mle; Naam, njoni, nunueni divai na maziwa, Bila fedha na bila thamani. |
2. | Kwani kutoa fedha kwa ajili ya kitu ambacho si chakula? Na mapato yenu kwa kitu kisichoshibisha? Nisikilizeni kwa bidii, mle kilicho chema, Na kujifurahisha nafsi zenu kwa unono. |
3. | Tegeni masikio yenu, na kunijia; Sikieni, na nafsi zenu zitaishi; Nami nitafanya nanyi agano la milele, Naam, rehema za Daudi zilizo imara. |
4. | Angalieni, nimemweka kuwa shahidi kwa kabila za watu; kuwa kiongozi na jemadari kwa kabila za watu. |
5. | Tazama, utaita taifa usilolijua, na taifa lisilokujua wewe litakukimbilia, kwa sababu ya Bwana, Mungu wako, na kwa ajili yake Mtakatifu wa Israeli; maana amekutukuza. |
6. | Mtafuteni Bwana, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; |
7. | Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa. |
8. | Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana. |
9. | Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu. |
10. | Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; |
11. | ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma. |
12. | Maana mtatoka kwa furaha, Mtaongozwa kwa amani; Mbele yenu milima na vilima vitatoa nyimbo; Na miti yote ya kondeni itapiga makofi. |
13. | Badala ya michongoma utamea msunobari, Na badala ya mibigili, mhadesi; Jambo hili litakuwa la kumpatia Bwana jina, Litakuwa ishara ya milele isiyokatiliwa mbali. |
← Isaiah (55/66) → |