Isaiah (54/66)  

1. Imba, wewe uliye tasa, wewe usiyezaa; paza sauti yako kwa kuimba, piga kelele, wewe usiyekuwa na utungu; maana watoto wake aliyeachwa ni wengi kuliko watoto wake yeye aliyeolewa, asema Bwana.
2. Panua mahali pa hema yako, na wayatandaze mapazia ya maskani yako; usiwakataze; ongeza urefu wa kamba zako; vikaze vigingi vya hema yako.
3. Kwa maana utaenea upande wa kuume na upande wa kushoto; na wazao wako watawamiliki mataifa; wataifanya miji iliyokuwa ukiwa kukaliwa na watu.
4. Usiogope; maana hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau aibu ya ujana wako, pia mashutumu ya ujane wako hutayakumbuka tena.
5. Kwa sababu Muumba wako ni mume wako; Bwana wa majeshi ndilo jina lake; na Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako; Yeye ataitwa Mungu wa dunia yote.
6. Maana Bwana amekuita kama mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni, kama mke wakati wa ujana, atupwapo, asema Mungu wako.
7. Kwa kitambo kidogo nimekuacha; lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya.
8. Kwa ghadhabu ifurikayo nalikuficha uso wangu dakika moja; lakini kwa fadhili za milele nitakurehemu, asema Bwana, Mkombozi wako.
9. Kwa maana jambo hili limekuwa kama maji ya Nuhu kwangu; maana kama nilivyoapa ya kwamba maji ya Nuhu hayatapita juu ya dunia tena, kadhalika nimeapa ya kwamba sitakuonea hasira, wala kukukemea.
10. Maana milima itaondoka, na vilima vitaondolewa; bali wema wangu hautaondoka kwako, wala agano langu la amani halitaondolewa; asema Bwana akurehemuye.
11. Ewe uliyeteswa, uliyerushwa na tufani, usiyetulizwa, tazama, nitaweka mawe yako kwa rangi nzuri, nitaweka misingi yako kwa yakuti samawi.
12. Nami nitaifanya minara yako ya akiki nyekundu, na malango yako ya almasi, na mipaka yako yote ya mawe yapendezayo.
13. Na watoto wako wote watafundishwa na Bwana; na amani ya watoto wako itakuwa nyingi.
14. Utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia.
15. Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako.
16. Tazama, nimemwumba mhunzi avukutaye moto wa makaa, akatoa silaha kwa kazi yake; nami nimemwumba mharibu ili aharibu.
17. Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.

  Isaiah (54/66)