| ← Isaiah (52/66) → | 
| 1. | Amka, amka, jivike nguvu zako, Ee Sayuni; Jivike mavazi yako mazuri, Ee Yerusalemu, mji mtakatifu; Kwa maana tokea sasa hataingia ndani yako Asiyetahiriwa, wala aliye najisi. | 
| 2. | Jikung'ute mavumbi; uondoke, Uketi, Ee Yerusalemu; Jifungulie vifungo vya shingo yako, Ee binti Sayuni uliyefungwa. | 
| 3. | Maana Bwana asema hivi, Mliuzwa bure; nanyi mtakombolewa bila fedha. | 
| 4. | Maana Bwana MUNGU asema hivi, Watu wangu hapo kwanza walishuka Misri ili wakae huko hali ya ugeni; na Mwashuri akawaonea bila sababu. | 
| 5. | Basi sasa, nafanya nini hapa, asema Bwana, ikiwa watu wangu wamechukuliwa bure? Hao wanaowatawala wanapiga yowe, asema Bwana, na jina langu linatukanwa daima mchana kutwa. | 
| 6. | Kwa hiyo watu wangu watalijua jina langu kwa hiyo watajua siku ile ya kuwa mimi ndimi ninenaye; tazama ni mimi. | 
| 7. | Jinsi ilivyo mizuri juu ya milima Miguu yake aletaye habari njema, Yeye aitangazaye amani, Aletaye habari njema ya mambo mema, Yeye autangazaye wokovu, Auambiaye Sayuni, Mungu wako anamiliki! | 
| 8. | Sauti ya walinzi wako! Wanapaza sauti zao, wanaimba pamoja; Maana wataona jicho kwa jicho, Jinsi Bwana arejeavyo Sayuni. | 
| 9. | Pigeni kelele za furaha, imbeni pamoja, Enyi mahali pa Yerusalemu palipokuwa ukiwa; Kwa kuwa Bwana amewafariji watu wake, Ameukomboa Yerusalemu. | 
| 10. | Bwana ameweka wazi mkono wake mtakatifu Machoni pa mataifa yote; Na ncha zote za dunia Zitauona wokovu wa Mungu wetu. | 
| 11. | Nendeni zenu, nendeni zenu, tokeni huko, msiguse kitu kichafu; tokeni kati yake; iweni safi ninyi mnaochukua vyombo vya Bwana. | 
| 12. | Maana hamtatoka kwa haraka, wala hamtakwenda kwa kukimbia, kwa sababu Bwana atawatangulia; na Mungu wa Israeli atawafuata nyuma; awalinde. | 
| 13. | Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa busara, atatukuzwa, na kuinuliwa juu, naye atakuwa juu sana. | 
| 14. | Kama vile wengi walivyokustaajabia, (uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu ye yote, na umbo lake zaidi ya wanadamu), | 
| 15. | ndivyo atakavyowasitusha mataifa mengi; wafalme watamfumbia vinywa vyao; maana mambo wasiyoambiwa watayaona; na mambo wasiyoyasikia watayafahamu. | 
| ← Isaiah (52/66) → |