← Isaiah (5/66) → |
1. | Na nimwimbie mpenzi wangu wimbo wa mpenzi wangu katika habari za shamba lake la mizabibu. Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu, Kilimani penye kuzaa sana; |
2. | Akafanya handaki kulizunguka pande zote, Akatoa mawe yake, Akapanda ndani yake mzabibu ulio mzuri, Akajenga mnara katikati yake, Akachimba shinikizo ndani yake; Akatumaini ya kuwa utazaa zabibu, Nao ukazaa zabibu-mwitu. |
3. | Na sasa, enyi wenyeji wa Yerusalemu, nanyi watu wa Yuda, amueni, nawasihi, kati ya mimi na shamba langu la mizabibu. |
4. | Je! Ni kazi gani iliyoweza kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu nisiyoitenda? Basi, nilipotumaini ya kuwa litazaa zabibu, mbona lilizaa zabibu-mwitu? |
5. | Haya basi, sasa nitawaambieni nitakalolitenda shamba langu la mizabibu; nitaondoa kitalu chake, nalo litaliwa; nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa; |
6. | nami nitaliharibu; wala halitapogolewa wala kulimwa, bali litamea mbigili na miiba; nami nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake. |
7. | Kwa maana shamba la mizabibu la Bwana wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza; akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe! Aliona dhuluma; alitumaini kuona haki, na kumbe! Alisikia kilio. |
8. | Ole wao waongezao nyumba baada ya nyumba, na kuweka shamba karibu na shamba, hata hapana nafasi tena, nanyi hamna budi kukaa peke yenu kati ya nchi! |
9. | Bwana wa majeshi asema katika masikio yangu, Hakika majumba mengi yatakuwa ukiwa, naam, majumba makubwa, mazuri, yatakuwa hayana watu. |
10. | Kwa maana shamba la mizabibu la eka kumi litatoa bathi moja tu, na homeri ya mbegu itatoa efa tu. |
11. | Ole wao waamkao asubuhi na mapema, wapate kufuata kileo; wakishinda sana hata usiku wa manane mpaka mvinyo imewaka kama moto ndani yao! |
12. | Na kinubi, na zeze, na matari, na filimbi, na mvinyo, zote ziko katika karamu zao; lakini hawaiangalii kazi ya Bwana wala kuyafikiri matendo ya mikono yake. |
13. | Kwa sababu hiyo watu wangu wamechukuliwa mateka, kwa kukosa kuwa na maarifa; na watu wao wenye cheo wana njaa, na wengi wao waona kiu sana. |
14. | Kwa hiyo kuzimu kumeongeza tamaa yake, kumefunua kinywa chake bila kiasi; na utukufu wao, na wingi wao, na ghasia yao, naye pia afurahiye miongoni mwao, hushuka na kuingia humo. |
15. | Na mtu mnyonge ainamishwa, na mtu mkubwa amedhilika, na macho yao walioinuka hunyenyekezwa, |
16. | bali Bwana wa majeshi ametukuzwa katika hukumu, na Mungu aliye Mtakatifu ametakaswa katika haki. |
17. | Ndipo wana-kondoo watakapolisha kama katika malisho yao wenyewe, na mahali pao waliowanda, palipoachwa ukiwa, wageni watakula. |
18. | Ole wao wavutao uovu kwa kamba za ubatili, na dhambi kama kwa kamba za gari! |
19. | Wasema, Na afanye haraka, aihimize kazi yake, tupate kuiona; na likaribie shauri lake aliye Mtakatifu wa Israeli, tupate kuliona. |
20. | Ole wao wasemao kwamba uovu ni wema, na kwamba wema ni uovu; watiao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza; watiao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu! |
21. | Ole wao walio wenye hekima katika macho yao wenyewe, na wenye busara katika fikira zao wenyewe! |
22. | Ole wao walio hodari kunywa kileo chenye nguvu, watu waume wenye nguvu kuchanganya vileo; |
23. | wampao haki mwenye uovu, ili wapewe ijara, na kumwondolea mwenye haki haki yake! |
24. | Kwa hiyo kama vile mwali wa moto uteketezavyo mabua makavu, na kama manyasi makavu yaangukavyo katika mwali wa moto; kadhalika shina lao litakuwa kama ubovu, na ua lao litapeperushwa juu kama mavumbi; kwa sababu wameikataa sheria ya Bwana wa majeshi, na kulidharau neno lake aliye Mtakatifu wa Israeli. |
25. | Kwa sababu hiyo hasira ya Bwana imewaka juu ya watu wake, naye amenyosha mkono wake juu yao; akawapiga, navyo vilima vilitetemeka, na mizoga yao ilikuwa kama takataka katika njia kuu. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa. |
26. | Naye atawatwekea bendera mataifa toka mbali, Naye atawapigia miunzi tokea mwisho wa nchi; Na tazama, watakuja mbio mbio upesi sana. |
27. | Miongoni mwao hakuna achokaye wala kukwaa; Hakuna asinziaye wala kulala usingizi; Wala mshipi wa viuno vyao hautalegea. Wala ukanda wa viatu vyao hautakatika; |
28. | Mishale yao ni mikali, na pindi zao zote zimepindika; Kwato za farasi zao zitahesabika kama gumegume; Na gurudumu zao kama kisulisuli; |
29. | Ngurumo yao itakuwa kama ya simba; Watanguruma kama wana-simba; Naam, watanguruma na kukamata mateka, Na kuyachukua na kwenda zao salama, Wala hakuna mtu atakayeokoa. |
30. | Nao watanguruma juu yao siku hiyo Kama ngurumo ya bahari; Na mtu akiitazama nchi, ataona giza na dhiki Nayo nuru imetiwa giza katika mawingu yake. |
← Isaiah (5/66) → |