← Isaiah (48/66) → |
1. | Sikieni haya, enyi watu wa nyumba ya Yakobo, mnaoitwa kwa jina la Israeli, mliotoka katika maji ya Yuda; mnaoapa kwa jina la Bwana, na kumtaja Mungu wa Israeli, lakini si kwa kweli, wala si kwa haki. |
2. | Maana hujiita wenyeji wa mji mtakatifu, hujitegemeza juu ya Mungu wa Israeli; Bwana wa majeshi ni jina lake. |
3. | Mimi nimehubiri mambo ya kale tangu zamani; naam, yalitoka katika kinywa changu, nikayadhihirisha; naliyatenda kwa ghafula, yakatokea. |
4. | Kwa sababu nalijua ya kuwa wewe u mkaidi, na shingo yako ni shingo ya chuma, na kipaji cha uso wako ni shaba; |
5. | basi nimekuonyesha tangu zamani; kabla hayajatukia nalikuonyesha; usije ukasema, Sanamu yangu imetenda haya; sanamu yangu ya kuchonga, na sanamu yangu ya kuyeyusha, imeyaamuru. |
6. | Umesikia haya; tazama haya yote; nanyi, je! Hamtayahubiri? Nimekuonyesha mambo mapya tangu wakati huu, naam, mambo yaliyofichwa, usiyoyajua. |
7. | Yameumbwa sasa, wala si tokea zamani; na kabla ya siku hii ya leo hukusikia habari yake; usije ukasema, Tazama, naliyajua. |
8. | Naam, hukusikia; naam, hukujua; naam, tokea zamani sikio lako halikuzibuka; maana nalijua ya kuwa wewe watenda kwa hila nyingi, nawe umeitwa mkosaji tangu kuzaliwa kwako; |
9. | kwa ajili ya jina langu nitaahirisha hasira yangu, na kwa ajili yako nitajizuia, ili nisifiwe, wala nisikukatilie mbali. |
10. | Tazama, nimekusafisha, lakini si kama fedha; nimekuchagua katika tanuru ya mateso. |
11. | Kwa ajili ya nafsi yangu, kwa ajili ya nafsi yangu, nitatenda haya; je! Litiwe unajisi jina langu? Wala sitampa mwingine utukufu wangu. |
12. | Nisikilize mimi, Ee Yakobo; na Israeli, niliyekuita; mimi ndiye. Mimi ni wa kwanza, na mimi ni wa mwisho pia. |
13. | Naam, mkono wangu umeuweka msingi wa dunia, na mkono wangu wa kuume umezitanda mbingu; niziitapo husimama pamoja. |
14. | Kusanyikeni, ninyi nyote, mkasikie; ni nani miongoni mwao aliyehubiri haya? Bwana amempenda; atatimiza mapenzi yake juu ya Babeli, na mkono wake utakuwa juu ya Wakaldayo. |
15. | Mimi, naam, mimi, nimenena; naam, nimemwita; nimemleta, naye ataifanikisha njia yake. |
16. | Nikaribieni, sikieni haya; tokea mwanzo sikunena kwa siri; tangu yalipokuwapo, mimi nipo; na sasa Bwana MUNGU amenituma, na roho yake. |
17. | Bwana, mkombozi wako, mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Mimi ni Bwana, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata. |
18. | Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari; |
19. | Tena wazao wako wangalikuwa kama mchanga, na hao waliotoka katika tumbo lako kama chembe zake; jina lake lisingalikatika, wala kufutwa mbele zangu. |
20. | Haya, tokeni katika Babeli, Kimbieni kutoka kwa Wakaldayo; Hubirini kwa sauti ya kuimba, tangazeni haya, Yatamkeni mpaka mwisho wa dunia, semeni, Bwana amemkomboa mtumishi wake, Yakobo. |
21. | Wala hawakuona kiu alipowaongoza jangwani; Alitoa maji katika mwamba kwa ajili yao; Pia akaupasua mwamba, maji yakatoka kwa nguvu. |
22. | Hapana amani kwa wabaya, asema Bwana. |
← Isaiah (48/66) → |