Isaiah (47/66)  

1. Haya, shuka, keti mavumbini, Ewe bikira, binti Babeli; Keti chini pasipo kiti cha enzi, Ewe binti wa Wakaldayo; Maana hutaitwa tena mwororo, mpenda anasa.
2. Twaa mawe ya kusagia, usage unga; Vua utaji wako, ondoa mavazi yako, Funua mguu wako, pita katika mito ya maji.
3. Uchi wako utafunuliwa, Naam, aibu yako itaonekana. Nitalipa kisasi; simkubali mtu ye yote.
4. Mkombozi wetu, Bwana wa majeshi ndilo jina lake, Mtakatifu wa Israeli.
5. Kaa kimya, ingia gizani, Ee binti wa Wakaldayo; Maana hutaitwa tena Malkia wa falme.
6. Nalikuwa nimekasirika na watu wangu, naliutia unajisi urithi wangu, nikawatia mkononi mwako; wewe hukuwatendea rehema; uliwatia wazee nira yako, nayo nzito sana.
7. Ukasema, Mimi nitakuwa bibi milele; hata hukuyatia hayo moyoni mwako, wala hukukumbuka mwisho wa mambo hayo.
8. Sasa, basi, sikia haya, wewe upendaye anasa, ukaaye na kujiona salama, wewe usemaye moyoni mwako, Mimi ndiye, wala hapana mwingine zaidi yangu mimi; sitaketi mfano wa mjane, wala sitajua kufiwa na watoto;
9. lakini mambo haya mawili yatakupata katika dakika moja siku moja, kufiwa na watoto, na ujane; yatakupata kiasi kitimilifu, uchawi wako ujapokuwa mwingi, na uganga wako mwingi mno.
10. Maana umeutumainia ubaya wako; umesema, Hapana anionaye; hekima yako, na maarifa yako yamekupotosha, nawe umesema moyoni mwako, Mimi ndiye, wala hapana mwingine zaidi yangu mimi.
11. Kwa sababu hiyo ubaya utakupata; wala hutajua kutopoa kwake; na msiba utakuangukia; hutaweza kuuondoa; na ukiwa utakupata kwa ghafula, usioujua.
12. Simama sasa na uganga wako, na wingi wa uchawi wako, uliojitaabisha nao tangu ujana wako; labda utaweza kupata faida, labda utaweza kushinda.
13. Umechoka kwa wingi wa mashauri yako; basi, na wasimame hao wajuao falaki, wazitazamao nyota, watabirio kila mwezi mambo ya mwezi huo, wakakuokoe na mambo yatakayokupata.
14. Tazama, watakuwa kama mabua makavu; moto utawateketeza; hawatajiokoa na nguvu za mwali wa moto; hautakuwa kaa la kukota moto, wala moto wa kukaa karibu nao.
15. Ndivyo yatakavyokuwa mambo hayo uliyojitaabisha nayo; wale waliofanya biashara nawe tangu ujana wako watatanga-tanga mbali nawe, kila mtu akienda zake; hapatakuwa na mtu wa kukuokoa.

  Isaiah (47/66)