Isaiah (46/66)  

1. Beli anaanguka chini, Nebo anainama; sanamu zao ziko juu ya wanyama, na juu ya ng'ombe; vitu vile mlivyokuwa mkivichukua huku na huku vimekuwa mzigo, mzigo wa kumlemea mnyama aliyechoka.
2. Wanajiinamisha, wanainama pamoja; hawakuweza kuutua mzigo, bali wao wenyewe wamekwenda kufungwa.
3. Nisikilizeni, enyi wa nyumba ya Yakobo, ninyi mlio mabaki ya nyumba ya Israeli, mliochukuliwa nami tangu tumboni, mlioinuliwa tangu mimbani;
4. na hata uzee wenu mimi ndiye, na hata wakati wenu wa mvi nitawachukueni; nimefanya, nami nitachukua; naam, nitachukua na kuokoa.
5. Mtanifananisha na nani, na kunisawazisha naye, na kunilinganisha naye, ili tuwe sawasawa?
6. Watu wamwagao dhahabu kutoka mfukoni, na kupima fedha katika mizani, huajiri mfua dhahabu, akaifanya mungu; huanguka, naam, huabudu.
7. Humchukua begani, humchukua, wakamsimamisha mahali pake, akasimama; hataondoka katika mahali pake, naam, mmoja atamwita, lakini hawezi kujibu, wala kumwokoa na taabu yake.
8. Kumbukeni haya, mkajionyeshe kuwa waume; jifahamisheni haya, ninyi mkosao;
9. kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi;
10. nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote.
11. Nikiita ndege mkali kutoka mashariki, mtu wa shauri langu toka nchi iliyo mbali; naam, nimenena, nami nitatekeleza; nimekusudia, nami nitafanya.
12. Nisikilizeni, ninyi mlio na moyo mshupavu, mlio mbali na haki;
13. Mimi ninaleta karibu haki yangu, haitakuwa mbali, na wokovu wangu hautakawia; nami nitaweka wokovu katika Sayuni kwa ajili ya Israeli, utukufu wangu.

  Isaiah (46/66)