← Isaiah (45/66) → |
1. | Haya ndiyo Bwana amwambiayo Koreshi, masihi |
2. | Nitakwenda mbele yako, na kupasawazisha mahali palipoparuza; nitavunja vipande vipande milango ya shaba, na kukata-kata mapingo ya chuma; |
3. | nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni Bwana, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli. |
4. | Kwa ajili ya Yakobo, mtumishi wangu, na Israeli, mteule wangu, nimekuita kwa jina lako; nimekupa jina la sifa; ijapokuwa hukunijua. |
5. | Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine; zaidi yangu mimi hapana Mungu; nitakufunga mshipi ijapokuwa hukunijua; |
6. | ili wapate kujua toka maawio ya jua, na toka magharibi, ya kuwa hapana mwingine zaidi ya mimi; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine. |
7. | Mimi naiumba nuru, na kulihuluku giza; mimi nafanya suluhu, na kuhuluku ubaya; Mimi ni Bwana, niyatendaye hayo yote. |
8. | Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, Mawingu na yamwage haki; Nchi na ifunuke, ili kutoa wokovu, Nayo itoe haki ikamee pamoja; Mimi, Bwana, nimeiumba. |
9. | Ole wake ashindanaye na Muumba wake! Kigae kimoja katika vigae vya dunia! Je! Udongo umwambie yeye aufinyangaye; Unafanya nini? Au kazi yako, Hana mikono? |
10. | Ole wake amwambiaye baba yake, Wazaa nini? Au mwanamke, Una utungu wa nini? |
11. | Bwana, Mtakatifu wa Israeli, na Muumba wake, asema hivi; Niulize habari za mambo yatakayokuja; mambo ya wana wangu, na habari ya kazi ya mikono yangu; haya! Niagizeni. |
12. | Mimi nimeiumba dunia, nimemhuluku mwanadamu juu yake; Mimi, naam, mikono yangu mimi, imezitanda mbingu, na jeshi lake lote nimeliamuru. |
13. | Mimi nimemwinua katika haki, nami nitazinyosha njia zake zote; ataujenga mji wangu, naye atawaacha huru watu wangu waliohamishwa, si kwa kulipwa fedha, wala kwa kupewa zawadi, asema Bwana wa majeshi. |
14. | Bwana asema hivi, Kazi ya Misri, na bidhaa ya Kushi, na Waseba, watu walio warefu, watakujilia, nao watakuwa wako; watakufuata; watakuja katika minyororo; wataanguka chini mbele yako, watakuomba, wakisema, Hakika Mungu yu ndani yako; wala hapana mwingine, hapana Mungu tena. |
15. | Hakika wewe u Mungu ujifichaye nafsi yako, Ee Mungu wa Israeli, Mwokozi. |
16. | Watatahayarika, naam, watafadhaika, wote pia; wale wafanyao sanamu wataingia fadhaa pamoja. |
17. | Bali Israeli wataokolewa na Bwana kwa wokovu wa milele; ninyi hamtatahayarika, wala kufadhaika, milele na milele. |
18. | Maana Bwana, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni Bwana, wala hapana mwingine. |
19. | Sikusema kwa siri, katika mahali pa nchi ya giza; sikuwaambia wazao wa Yakobo; Nitafuteni bure; Mimi, Bwana, nasema haki; nanena mambo ya adili. |
20. | Jikusanyeni mje; na kukaribia pamoja, ninyi wa mataifa mliookoka; hawana maarifa wale wachukuao mti wa sanamu yao ya kuchonga; wamwombao mungu asiyeweza kuokoa. |
21. | Hubirini, toeni habari; naam, na wafanye mashauri pamoja; ni nani aliyeonyesha haya tangu zamani za kale? Ni nani aliyeyahubiri hapo zamani? Si mimi, Bwana? Wala hapana Mungu zaidi ya mimi; Mungu mwenye haki, mwokozi; hapana mwingine zaidi ya mimi. |
22. | Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni Mungu; hapana mwingine. |
23. | Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa. |
24. | Mmoja ataniambia, Kwa Bwana, peke yake, iko haki na nguvu; naam, watu watamwendea yeye, na wote waliomkasirikia watatahayarika. |
25. | Katika Bwana wazao wote wa Israeli watapewa haki, na kutukuka. |
← Isaiah (45/66) → |