← Isaiah (44/66) → |
1. | Lakini sikia sasa, Ee Yakobo, mtumishi wangu; na Israeli, niliyekuchagua; |
2. | Bwana, aliyekufanya, na kukuumba toka tumboni, yeye atakayekusaidia, asema hivi; Usiogope, Ee Yakobo, mtumishi wangu; na wewe, Yeshuruni, niliyekuchagua. |
3. | Kwa maana nitamimina maji juu yake aliye na kiu, na vijito vya maji juu ya mahali pakavu; nitamwaga roho yangu juu ya wazao wako, na baraka yangu juu yao utakaowazaa; |
4. | nao watatokea katika manyasi, kama mierebi karibu na mifereji ya maji. |
5. | Mmoja atasema, Mimi ni wa Bwana; na mwingine atajiita kwa jina la Yakobo; na mwingine ataandika juu ya mkono wake, Kwa Bwana, na kujiita kwa jina la Israeli. |
6. | Bwana, Mfalme wa Israeli, Mkombozi wako, Bwana wa majeshi, asema hivi; Mimi ni wa kwanza, na mimi ni wa mwisho; zaidi yangu mimi hapana Mungu. |
7. | Naye ni nani kama mimi atakayeita, na kuyahubiri haya, na kunitengenezea, tangu nilipowaweka watu wa kale? Na mambo yanayokuja na yatakayotokea, wayatangaze. |
8. | Msiogope wala msifanye hofu; je! Sikukuhubiri haya zamani na kuyaonyesha? Na ninyi ni mashahidi wangu. Je! Yuko Mungu zaidi yangu mimi? Hakika hapana Mwamba; mimi sijui mwingine. |
9. | Wachongao sanamu, wote ni ubatili; wala mambo yao yawapendezayo hayatafaa kitu; wala mashahidi wao wenyewe hawaoni, wala hawajui; ili watahayarike. |
10. | Ni nani aliyejichongea mungu mmoja, au aliyesubu sanamu isiyofaa kitu? |
11. | Tazama, wenziwe wote watatahayari; na mafundi, hao ni wanadamu; na wakusanyike pamoja, wakasimame; wataogopa na kutahayari pamoja. |
12. | Mfua chuma hufanza shoka, hufanya kazi kwa makaa, huitengeneza sanamu kwa nyundo, huifanyiza kwa nguvu za mkono wake; naam, huona njaa, nguvu zake zikampungukia; asipokunywa maji huzimia. |
13. | Seremala hunyosha uzi; huiandika kwa kalamu ya mate; huitengeneza kwa randa, huiandika kwa bikari, huifanza kwa mfano wa mwanadamu, sawasawa na uzuri wa mwanadamu, ili ikae nyumbani. |
14. | Yeye hujikatia mierezi, hutwaa mtiriza, na mwaloni, hujichagulia mti mmoja katika miti ya msituni; hupanda mvinje, mvua ikausitawisha. |
15. | Kisha utamfaa mwanadamu kwa kuni; hutwaa kipande, akaota moto; naam, huuwasha moto, akaoka mkate; naam, huufanya mungu, akauabudu; huifanya sanamu ya kuchonga, akaisujudia. |
16. | Sehemu moja huiteketeza; kwa sehemu nyingine hula nyama; huoka chakula kiokwacho, akashiba; naam, huota moto, akasema, Aha, nimeota moto, nimeona moto; |
17. | na kwa sehemu iliyobakia hufanya mungu, yaani, sanamu yake ya kuchonga; husujudu mbele yake akaiabudu, akaiomba, akasema, Uniokoe; maana wewe u mungu wangu. |
18. | Hawajui wala hawafikiri; maana amewafumba macho, wasione, na mioyo yao, wasiweze kufahamu. |
19. | Wala hapana atiaye moyoni, wala hapana maarifa, wala fahamu kusema, Nimeteketeza sehemu motoni, naam, pia nimeoka mkate juu ya makaa yake; nimeoka nyama nikaila; nami, je! Kilichobaki nikifanye kuwa chukizo? Je! Nisujudie shina la mti? |
20. | Hula majivu; moyo uliodanganyika umempotosha, asiweze kuiokoa nafsi yake, wala kusema, Je! Sio uongo mkononi mwangu? |
21. | Kumbuka haya, Ee Yakobo; nawe Israeli, maana wewe u mtumishi wangu; nimekuumba; u mtumishi wangu; Ee Israeli, hutasahauliwa na mimi. |
22. | Nimeyafuta makosa yako kama wingu zito, na dhambi zako kama wingu; unirudie; maana nimekukomboa. |
23. | Imbeni, enyi mbingu, maana Bwana ametenda hayo; Pigeni kelele, enyi mabonde ya nchi; Pazeni nyimbo, enyi milima; Nawe, msitu, na kila mti ndani yake. Maana Bwana amemkomboa Yakobo, Naye atajitukuza katika Israeli. |
24. | Bwana, mkombozi wako, yeye aliyekuumba tumboni, asema hivi; Mimi ni Bwana, nifanyaye vitu vyote; nizitandaye mbingu peke yangu; niienezaye nchi; ni nani aliye pamoja nami? |
25. | Nizitanguaye ishara za waongo, na kuwatia waganga wazimu; niwarudishaye nyuma wenye hekima, na kuyageuza maarifa yao kuwa ujinga; |
26. | nilithibitishaye neno la mtumishi wangu, na kuyafikiliza mashauri ya wajumbe wangu; niuambiaye Yerusalemu, Utakaliwa na watu, nayo miji ya Yuda, Itajengwa, nami nitapainua mahali pake palipobomoka; |
27. | niviambiaye vilindi, Kauka, nami nitaikausha mito yako; |
28. | nimwambiaye Koreshi, Mchungaji wangu, naye atayatenda mapenzi yangu; hata ataunena Yerusalemu, Utajengwa; na hilo hekalu, Msingi wako utawekwa. |
← Isaiah (44/66) → |