← Isaiah (42/66) → |
1. | Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu. |
2. | Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu. |
3. | Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli. |
4. | Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake. |
5. | Mungu Bwana anena, yeye aliyeziumba mbingu, na kuzitanda; yeye aliyeitandaza nchi na mazao yake; yeye awapaye pumzi watu walio juu yake; yeye awapaye roho wao waendao ndani yake. |
6. | Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa; |
7. | kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa. |
8. | Mimi ni Bwana; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu. |
9. | Tazama, mambo ya kwanza yamekuwa, nami nayahubiri mambo mapya; kabla hayajatokea nawapasheni habari zake. |
10. | Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Na sifa zake tokea mwisho wa dunia; Ninyi mshukao baharini, na vyote vilivyomo, Na visiwa, nao wakaao humo. |
11. | Jangwa na miji yake na ipaze sauti zao, Vijiji vinavyokaliwa na Kedari; Na waimbe wenyeji wa Sela, Wapige kelele toka vilele vya milima. |
12. | Na wamtukuze Bwana, Na kutangaza sifa zake visiwani. |
13. | Bwana atatokea kama shujaa; Ataamsha wivu kama mtu wa vita; Atalia, naam, atapiga kelele; Atawatenda adui zake mambo makuu. |
14. | Siku nyingi nimenyamaza kimya; nimenyamaza, nikajizuia; sasa nitapiga kelele kama mwanamke aliye katika kuzaa; nitaugua na kutweta pamoja. |
15. | Nitaharibu milima na vilima, nitavikausha vyote vimeavyo; nitaifanya mito ya maji kuwa visiwa, na kuyakausha maziwa ya maji. |
16. | Nitawaleta vipofu kwa njia wasiyoijua; katika mapito wasiyoyajua nitawaongoza; nitafanya giza kuwa nuru mbele yao; na mahali palipopotoka kuwa pamenyoka. Haya nitayatenda, wala sitawaacha. |
17. | Watarudishwa nyuma, wataaibishwa sana, hao wanaotumainia sanamu za mawe, na kuziambia sanamu za madini, Ninyi ndinyi miungu yetu. |
18. | Sikilizeni, enyi viziwi; tazameni, enyi vipofu, mpate kuona. |
19. | Ni nani aliye kipofu, ila mtumishi wangu? Au aliye kiziwi, kama mjumbe wangu nimtumaye? Ni nani aliye kipofu, kama yeye aliye na amani? Naam, kipofu kama mtumishi wa Bwana? |
20. | Unaona mambo mengi, lakini huyatii moyoni; masikio yake ya wazi, lakini hasikii. |
21. | Bwana akapendezwa, kwa ajili ya haki yake, kuitukuza sheria, na kuiadhimisha. |
22. | Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha. |
23. | Ni nani miongoni mwenu atakayetega sikio lake kuyasikia hayo? Atakayesikiliza na kusikia kwa wakati ujao? |
24. | Ni nani aliyemtoa Yakobo awe mateka, aliyemtia Israeli katika mikono ya wanyang'anyi? Si yeye, Bwana? Yeye tuliyemkosa, ambaye hawakutaka kwenda katika njia zake, wala hawakuitii sheria yake. |
25. | Kwa sababu hiyo alimwaga ukali wa hasira yake juu yake, na nguvu za vita; ukawasha moto wa kumzunguka pande zote, wala hakujua; ukamteketeza, wala hakuyatia hayo moyoni mwake. |
← Isaiah (42/66) → |