← Isaiah (41/66) → |
1. | Nyamazeni mbele zangu, enyi visiwa, na mataifa wajipatie nguvu mpya; na waje karibu wakanene; na tukaribiane pamoja kwa hukumu. |
2. | Ni nani aliyemwinua mmoja atokaye mashariki, ambaye katika haki amemwita mguuni pake? Ampa mataifa mbele yake, na kumtawaza juu ya wafalme; awatoa wawe kama mavumbi kwa upanga wake, kama makapi yaliyopeperushwa kwa upinde wake. |
3. | Awafuatia, apita salama hata kwa njia asiyoikanyaga kamwe kwa miguu yake. |
4. | Ni nani aliyetenda na kufanya jambo hilo, aviitaye vizazi tangu mwanzo? Mimi, Bwana, wa kwanza na wa mwisho, mimi ndiye. |
5. | Visiwa vimeona, vikaogopa; ncha za dunia zilitetemeka; walikaribia, walikuja. |
6. | Wakasaidiana, kila mtu na mwenzake, kila mtu akamwambia ndugu yake; Uwe na moyo mkuu. |
7. | Seremala akamtia moyo mfua dhahabu, na yeye alainishaye kwa nyundo akamhimiza yule apigaye fuawe, akiisifu kazi ya kuunga, akisema, Ni kazi njema; naye akaikaza kwa misumari isitikisike. |
8. | Nawe, Israeli, mtumishi wangu; Yakobo, niliyekuchagua; mzao wa Ibrahimu, rafiki yangu; |
9. | wewe niliyekushika toka miisho ya dunia, na kukuita toka pembe zake, nikikuambia, Wewe u mtumishi wangu; nimekuchagua wala sikukutupa; |
10. | usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. |
11. | Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. |
12. | Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. |
13. | Kwa maana mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia. |
14. | Usiogope, Yakobo uliye mdudu, nanyi watu wa Israeli; mimi nitakusaidia, asema Bwana, na mkombozi wako ni Mtakatifu wa Israeli. |
15. | Tazama, nitakufanya kuwa chombo kikali kipya cha kupuria, chenye meno; utaifikicha milima, na kuisaga; nawe utafanya vilima kuwa kama makapi. |
16. | Utawapepeta, na upepo utawapeperusha; upepo wa kisulisuli utawatawanya; nawe utamfurahia Bwana, utajitukuza katika Mtakatifu wa Israeli. |
17. | Maskini na wahitaji wanatafuta maji, wala hapana; ndimi zao zimekauka kwa kiu; mimi, Bwana, nitawasikia, mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha. |
18. | Nitafunua vijito vya maji juu ya vilima, na chemchemi katikati ya mabonde; nitageuza jangwa kuwa ziwa la maji, na mahali pakavu kuwa vijito vya maji. |
19. | Nitapanda katika jangwa mwerezi, mshita, mhadasi, na mbono; nitatia katika nyika mberoshi, mtidhari, na mteashuri pamoja; |
20. | ili waone, na kujua, wakafikiri, na kufahamu pamoja, ya kuwa mkono wa Bwana ndio uliofanya jambo hilo. Mtakatifu wa Israeli ndiye aliyeliumba. |
21. | Haya, leteni maneno yenu, asema Bwana; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo. |
22. | Wayatangaze na kutujulisha yatakayokuwa; watuonyeshe mambo ya zamani, ni mambo gani, tukapate kuyatia moyoni, tukajue mwisho wake; au wamdhihirishie yatakayotokea baadaye. |
23. | Tujulisheni yatakayokuwa baadaye, nasi tutakiri ya kuwa ninyi ni miungu; naam, tendeni mema au tendeni mabaya, ili tujipime, tukaone pamoja. |
24. | Tazameni, ninyi si kitu, tena kazi yenu si kitu; awachaguaye ninyi ni chukizo. |
25. | Nimemwinua mtu toka kaskazini, naye amekuja; toka maawio ya jua amekuja anitajaye jina langu; naye atawajilia maliwali kama akanyagaye matope, na kama mfinyanzi afinyangaye udongo. |
26. | Ni nani aliyeihubiri habari tokea mwanzo, tupate kuijua? Na tokea zamani, tupate kusema, Yeye ni mwenye haki? Naam, hapana hata mmoja aliyetujulisha; naam, hapana hata mmoja aliyetuonyesha; naam, hapana hata mmoja aliyesikia maneno yenu. |
27. | Mimi kwanza nitauambia Sayuni, Tazama; hawa ndio; nami nitampa Yerusalemu mletaji wa habari njema. |
28. | Na nitazamapo, hapana mtu, hata katika watu hao hapana mshauri mmoja, ambaye, nikimwuliza, aweza kunijibu neno. |
29. | Tazama, hao wote ni ubatili; kazi zao si kitu; sanamu zao ni upepo na fujo. |
← Isaiah (41/66) → |