← Isaiah (37/66) → |
1. | Ikawa mfalme Hezekia aliposikia hayo, alizirarua nguo zake, akajivika nguo za magunia, akaingia katika nyumba ya Bwana. |
2. | Akamtuma Eliakimu aliyekuwa msimamizi wa nyumba yake na Shebna, mwandishi, na wazee wa makuhani, wamejivika nguo za magunia, waende kwa Isaya nabii, mwana wa Amozi. |
3. | Wakamwambia, Hezekia asema hivi, Siku hii ni siku ya dhiki, na aibu, na matukano; maana watoto wa tayari kuzaliwa, wala hapana nguvu za kuwazaa. |
4. | Yamkini Bwana, Mungu wako, atayasikia maneno ya huyo amiri ambaye mfalme wa Ashuru, bwana wake, amemtuma ili amtukane Mungu aliye hai; na Bwana, Mungu wako atayakemea maneno aliyoyasikia; basi, inua dua yako kwa ajili ya mabaki yaliyobakia. |
5. | Basi, watumishi wa mfalme Hezekia wakaenda kwa Isaya. |
6. | Isaya akawaambia, Mwambieni bwana wenu maneno haya; Bwana asema hivi, Usiyaogope maneno uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana. |
7. | Tazama, nitatia roho ndani yake, naye atasikia kivumi, na kurudi hata nchi yake mwenyewe, nami nitamwangusha kwa upanga katika nchi yake mwenyewe. |
8. | Basi yule amiri akarudi, akamkuta mfalme wa Ashuru anafanya vita juu ya Libna; kwa maana alikuwa amesikia ya kwamba ameondoka, akaacha Lakishi. |
9. | Naye alisikia habari ya Tirhaka, mfalme wa Kushi, ya kwamba, Ametoka ili kupigana nawe; naye aliposikia hayo, akatuma wajumbe kwa Hezekia, kusema, |
10. | Mwambieni Hezekia, mfalme wa Yuda, maneno haya, mkisema, Asikudanganye Mungu wako unayemtumaini, akisema, Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme wa Ashuru. |
11. | Tazama, umesikia habari ya mambo yote, ambayo wafalme wa Ashuru wamezitenda nchi zote, kwa kuziangamiza kabisa je! Utaokoka wewe? |
12. | Je! Miungu ya mataifa, ambao baba zangu waliwaangamiza, wamewaokoa? Gozani, na Harani, na Resefu, na wana wa Adini waliokuwa katika Telasari? |
13. | Yuko wapi mfalme wa Hamathi, na mfalme wa Arpadi, na mfalme wa mji wa Sefarvaimu, wa Hena, na wa Iva? |
14. | Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya Bwana, akaukunjua mbele za Bwana. |
15. | Hezekia akamwomba Bwana, akisema, |
16. | Ee Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia. Wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi. |
17. | Tega sikio lako, Bwana, usikie; funua macho yako, Bwana, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, aliyopeleka ili kumtukana Mungu aliye hai. |
18. | Ni kweli, Bwana, wafalme wa Ashuru wameziharibu nchi zote, na mashamba yao, |
19. | na kuwatupa miungu yao motoni; kwa maana hao hawakuwa miungu, bali kazi ya mikono ya wanadamu; walikuwa miti na mawe, ndiyo sababu wakawaharibu. |
20. | Basi sasa, Bwana, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe Bwana, wewe peke yako. |
21. | Ndipo Isaya, mwana wa Amozi, akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akisema, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa umeniomba juu ya Senakeribu, mfalme wa Ashuru, |
22. | tamko alilolitamka Bwana katika habari zake ndilo hili; Bikira, binti Sayuni, anakudharau, anakudhihaki sana; binti Yerusalemu anatikisa kichwa chake juu yako. |
23. | Ni nani uliyemshutumu na kumtukana? Umeinua sauti yako juu ya nani, na kuinua macho yako juu? Juu ya Mtakatifu wa Israeli. |
24. | Umemshutumu Bwana kwa watumishi wako, kwa kuwa umesema, Kwa wingi wa magari yangu nimepanda juu ya vilele vya milima, mpaka mahali pa ndani ya Lebanoni; nami nitaikata mierezi yake mirefu, na misunobari yake mizuri, nami nitaingia ndani ya mahali pake palipoinuka, palipo mbali sana, msitu wa shamba lake lizaalo sana. |
25. | Nimechimba na kunywa maji, na kwa nyayo za miguu yangu nitaikausha mito yote ya Misri. |
26. | Je! Hukusikia? Ni mimi niliyeyatenda hayo tokea zamani, na kuyafanya tokea siku za kale; nikayatimiza sasa, iwe kazi yako kuangamiza miji yenye boma, ikawe chungu na magofu. |
27. | Ndiyo sababu wenyeji wao wakawa hawana nguvu, na kufadhaika, na kuhangaika, wakawa kama majani ya mashamba, kama miche mibichi, kama majani juu ya dari, kama shamba la ngano kabla haijaiva. |
28. | Lakini nakujua, kuketi kwako, na kutoka kwako, na kuingia kwako; na ghadhabu yako uliyonighadhibikia. |
29. | Kwa sababu ya kunighadhibikia kwako, na kwa sababu kutakabari kwako kumefika masikioni mwangu, nitatia kulabu yangu katika pua yako, na hatamu yangu midomoni mwako, nami nitakurudisha kwa njia ile ile uliyoijia. |
30. | Na kwako wewe dalili ndiyo hii; mwaka huu mtakula vitu vimeavyo vyenyewe; na mwaka wa pili mtakula mazao ya mbegu za vitu hivyo; na mwaka wa tatu pandeni mbegu, kavuneni; mkapande mizabibu katika mashamba, mkale matunda yake. |
31. | Na mabaki yaliyookoka, yaliyobakia ya nyumba ya Yuda, yatatia mizizi chini, na kuzaa matunda juu. |
32. | Maana katika Yerusalemu yatatoka mabaki, nao watakaookoka katika mlima Sayuni; wivu wa Bwana wa majeshi utatimiza mambo hayo. |
33. | Basi, Bwana asema hivi katika habari za mfalme wa Ashuru, Yeye hataingia ndani ya mji huu, wala hatapiga mshale hapa, wala hatakuja mbele yake kwa ngao, wala hatajenga boma juu yake. |
34. | Njia ile ile aliyoijia, kwa njia hiyo atarudi zake, wala hataingia ndani ya mji huu; asema Bwana. |
35. | Nami nitaulinda mji huu, niuokoe kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu. |
36. | Basi malaika wa Bwana alitoka, akaua watu mia na themanini na tano elfu katika kituo cha Waashuri, na watu walipoamka asubuhi na mapema, kumbe, hao walikuwa maiti wote pia. |
37. | Basi Senakeribu, mfalme wa Ashuru akaenda zake, akarudi Ninawi, akakaa huko. |
38. | Ikawa alipokuwa akiabudu katika nyumba ya Nisroki, mungu wake, Adrameleki na Shareza, wanawe, wakampiga kwa upanga; wakakimbilia nchi ya Ararati; naye Esar-hadoni, mwanawe, akamiliki badala yake. |
← Isaiah (37/66) → |