Isaiah (34/66)  

1. Karibuni, enyi mataifa, mpate kusikia; sikilizeni, enyi kabila za watu; dunia na isikie, nacho kiijazacho, ulimwengu na vitu vyote viutokavyo.
2. Maana Bwana ana ghadhabu juu ya mataifa yote, na hasira kali juu ya jeshi lao lote; amewaangamiza kabisa, amewatoa waende kuchinjwa.
3. Watu wao waliouawa watatupwa nje, na uvundo wa maiti zao utapaa juu, na milima itayeyushwa kwa damu yao.
4. Na jeshi lote la mbinguni litafumuliwa, na mbingu zitakunjwa kama karatasi, na jeshi lao lote litanyauka kama vile jani la mzabibu linyaukavyo na kupukutika, na kama jani la mtini linyaukavyo na kupukutika.
5. Maana upanga wangu umekunywa na kushiba mbinguni; tazama, utashukia Edomu, na juu ya watu wa laana yangu, ili kuwahukumu.
6. Upanga wa Bwana umeshiba damu, umenona kwa unono, kwa damu ya wana-kondoo na mbuzi, kwa mafuta ya figo za kondoo waume; maana Bwana ana dhabihu huko Bozra, machinjo makubwa katika nchi ya Edomu.
7. Na nyati watatelemka pamoja nao, na mahasai pamoja na mafahali, na nchi yao italewa kwa damu, na mavumbi yake yatanoneshwa kwa shahamu.
8. Maana ni siku ya kisasi cha Bwana, mwaka wa malipo, ili kushindania Sayuni.
9. Na vijito vyake vitageuzwa kuwa lami, na mavumbi yake yatageuzwa kuwa kiberiti, na ardhi yake itakuwa lami iwakayo.
10. Haitazimwa mchana wala usiku, moshi wake utapaa milele; tangu kizazi hata kizazi itakuwa ukiwa; hapana mtu atakayepita kati yake milele na milele.
11. Kaati na nungu wataimiliki, bundi na kunguru watakaa huko, naye atanyosha juu yake kamba ya ukiwa na timazi ya utupu.
12. Watawaitia wakuu wake ufalme, lakini hawatakuwapo; wakuu wake wote wamekuwa si kitu.
13. Miiba itamea majumbani mwake, upupu na mbigili ndani ya maboma yake; nayo itakuwa kao la mbweha, na ua la mbuni.
14. Na hayawani wa nyikani watakutana na mbwa-mwitu, na beberu anamwita mwenziwe; naam, babewatoto anakaa huko na kujipatia raha.
15. Huko pili atafanya kioto chake na kuzaa na kuotamia, na kukusanya watoto wake katika kivuli chake; naam, huko watakusanyika tai, kila mmoja na mwenzake.
16. Tafuteni katika kitabu cha Bwana mkasome; hapana katika hao wote atakayekosa kuwapo, hapana mmoja atakayemkosa mwenzake; kwa maana kinywa changu kimeamuru, na roho yake imewakusanya.
17. Naye amewapigia kura, na mkono wake umewagawanyia kwa kamba; wataimiliki hata milele, watakaa ndani yake kizazi hata kizazi.

  Isaiah (34/66)