Isaiah (33/66)  

1. Ole wako uharibuye ila hukuharibiwa, utendaye hila wala hukutendwa hila! Utakapokwisha kuharibu, utaharibiwa wewe; na utakapokwisha kutenda kwa hila, wao watakutenda hila wewe.
2. Ee Bwana, uturehemu; tumekungoja wewe; uwe wewe mkono wetu
3. Kabila za watu wamekimbia wakisikia kelele za fujo; mataifa wametawanyika ulipojiinua nafsi yako.
4. Na mateka yako yatakumbwa kama wadudu wakumbavyo, wataruka juu yake kama arukavyo nzige.
5. Bwana ametukuka; kwa maana anakaa juu; amejaza Sayuni hukumu na haki.
6. Nyakati zako zitakuwa nyakati za kukaa imara; za wokovu tele na hekima na maarifa; kumcha Bwana ni hazina yake ya akiba.
7. Angalia, mashujaa wao wanalia nje, wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu.
8. Njia kuu zimeachwa, msafiri amekoma; ameyavunja maagano, ameidharau miji, hamjali mtu.
9. Nchi inaomboleza, na kulegea; Lebanoni imetahayarika na kunyauka; Sharoni imekuwa kama jangwa; Bashani na Karmeli zimepukutika majani.
10. Basi, sasa nitasimama; asema Bwana; sasa nitajiinua, sasa nitajitukuza.
11. Ninyi mtachukua mimba ya makapi, mtazaa majani makavu; pumzi yenu ni moto utakaowateketeza wenyewe.
12. Nao mataifa watakuwa kama kuchoma chokaa, kama miiba iliyokatika, iteketezwayo motoni.
13. Sikieni, ninyi mlio mbali, niliyoyatenda; na ninyi mlio karibu, kirini uweza wangu.
14. Wenye dhambi walio katika Sayuni wanaogopa; tetemeko limewashika wasiomcha Mungu; Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto ulao; ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele?
15. Ni yeye aendaye kwa haki, anenaye maneno ya adili; ni yeye anayedharau faida ipatikanayo kwa dhuluma; akung'utaye mikono yake asipokee rushwa; azibaye masikio yake asisikie habari za damu; afumbaye macho yake asitazame uovu.
16. Huyu ndiye atakayekaa juu; majabali ni ngome yake; atapewa chakula chake; maji yake hayatakoma.
17. Macho yako yatamwona mfalme katika uzuri wake, yataona nchi iliyoenea sana.
18. Moyo wako utatafakari hofu ile; Yuko wapi yeye aliyehesabu? Yuko wapi yeye aliyeupima ushuru? Yuko wapi yeye aliyeihesabu minara?
19. Hutawaona watu wale wakali; watu wa maneno magumu usiyoweza kuyafahamu; wenye lugha ya kigeni usiyoweza kuelewa nayo.
20. Angalia Sayuni, mji wa sikukuu zetu; macho yako yatauona Yerusalemu umekuwa kao la raha; hema isiyotanga-tanga; vigingi vyake havitang'olewa, wala kamba zake hazitakatika.
21. Bali huko Bwana atakuwa pamoja nasi, mwenye adhama; mahali penye mito mipana na vijito, pasipopita mashua na makasia yake; wala hapana merikebu ya vita itakayopita hapo.
22. Kwa maana Bwana ndiye mwamuzi wetu; Bwana ndiye mfanya sheria wetu; Bwana ndiye mfalme wetu; ndiye atakayetuokoa.
23. Kamba zako zimelegea; hawakuweza kukaza sana shina la mlingoti wao; hawakuweza kulikunjua tanga; ndipo mapato ya mateka yaligawanywa, hata wachechemeao walipata mateka.
24. Wala hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa; watu wakaao humo watasamehewa uovu wao.

  Isaiah (33/66)