Isaiah (31/66)  

1. Ole wao watelemkao kwenda Misri wapate msaada, na kutegemea farasi; watumainio magari kwa kuwa ni mengi, na wapanda farasi kwa kuwa ni hodari sana; lakini hawamwangalii Mtakatifu wa Israeli, wala hawamtafuti Bwana!
2. Lakini yeye naye ana akili, naye ataleta uovu, wala hatayatangua maneno yake; bali ataondoka juu ya nyumba yao watendao mabaya, na juu ya msaada wa hao watendao maovu.
3. Basi Wamisri ni wanadamu wala si Mungu, na farasi zao ni nyama wala si roho; na Bwana atakaponyosha mkono wake, yeye asaidiaye atajikwaa, na yeye asaidiwaye ataanguka, nao wote pamoja watakoma.
4. Maana Bwana aniambia hivi, Kama vile ilivyo simba angurumapo na mwana-simba juu ya mawindo yake, wachungaji wengi wakiitwa ili kumpiga, lakini hatiwi hofu na sauti zao, wala kufanya woga kwa sababu ya mshindo wao; ndivyo Bwana wa majeshi atakavyoshuka ili kufanya vita juu ya mlima Sayuni, na juu ya kilima chake.
5. Kama ndege warukao, Bwana wa majeshi ataulinda Yerusalemu; ataulinda na kuuokoa, atapita juu yake na kuuhifadhi.
6. Mwelekeeni yeye mliyemwasi sana, enyi wana wa Israeli.
7. Maana katika siku hiyo kila mtu atatupa sanamu zake za fedha, na sanamu zake za dhahabu, ambazo mikono yenu imezifanya, zikawa dhambi kwenu.
8. Ndipo huyo Mwashuri ataanguka kwa upanga ambao si wa mtu; na upanga usio upanga wa mtu utamla; naye ataukimbia upanga, na vijana wake watatoa kodi.
9. Na mwamba wake utatoweka kwa sababu ya hofu, nao wakuu wake wataionea bendera hofu kuu, asema Bwana, ambaye moto wake u katika Sayuni, na tanuru yake katika Yerusalemu.

  Isaiah (31/66)