← Isaiah (3/66) → |
1. | Kwa maana, tazama, Bwana, Bwana wa majeshi, awaondolea Yerusalemu na Yuda egemeo na tegemeo; tegemeo lote la chakula na tegemeo lote la maji; |
2. | mtu hodari na mtu wa vita; mwamuzi na nabii; mpiga ramli na mzee; |
3. | jemadari aliye juu ya watu hamsini, na mtu mstahifu, na mshauri, na fundi aliye mstadi, na mganga ajuaye uganga sana. |
4. | Nami nitawapa watoto kuwamiliki, na watoto wachanga kuwatawala. |
5. | Nao watu wataonewa, kila mtu na mwenziwe, na kila mtu na jirani yake; mtoto atajivuna mbele ya mzee, na mtu mnyonge mbele ya mtu mwenye heshima. |
6. | Mtu atakapomshika ndugu yake ndani ya nyumba ya baba yake, akisema, Wewe una nguo, ututawale wewe; na mahali hapa palipobomoka pawe chini ya mkono wako; |
7. | basi, siku ile atainua sauti yake, akisema, Mimi sitakuwa mponya watu; kwa maana ndani ya nyumba yangu hamna chakula wala mavazi; wala hamtanifanya kuwa mtawala juu ya watu hawa. |
8. | Kwa maana Yerusalemu umebomolewa na Yuda wameanguka, kwa sababu ulimi wao na matendo yao ni kinyume cha Bwana, hata wayachukize macho ya utukufu wake. |
9. | Kuonekana kwa nyuso zao kwashuhudia juu yao, wafunua dhambi yao kama Sodoma, hawaifichi. Ole wa nafsi zao, kwa maana wamejilipa nafsi zao uovu. |
10. | Waambieni wenye haki ya kuwa watakuwa heri, kwa maana watakula matunda ya matendo yao |
11. | Ole wake mtu mbaya; shari itakuwa kwake, kwa maana atapewa ijara ya mikono yake. |
12. | Katika habari za watu wangu, watoto ndio wanaowaonea, na wanawake ndio wanaowatawala. Enyi watu wangu, wakuongozao wakukosesha, waiharibu njia ya mapito yako. |
13. | Bwana asimama ili atete, asimama ili awahukumu watu. |
14. | Bwana ataingia katika kuwahukumu wazee wa watu wake na wakuu wao; Ninyi ndinyi mliokula shamba la mizabibu; vitu mlivyowateka maskini vi ndani ya nyumba zenu. |
15. | Ni nini maana yake, ninyi kuwaonea watu wangu, na kuseta nyuso za maskini? Asema Bwana, Bwana wa majeshi. |
16. | Bwana akasema tena, Kwa sababu binti za Sayuni wana kiburi, na kuenenda na shingo zilizonyoshwa, na macho ya kutamani, wakienenda kwa hatua za madaha, na kuliza njuga kwa miguu yao; |
17. | Basi, kwa hiyo, Bwana atawapiga binti za Sayuni kwa pele za utosini, na Bwana ataifunua aibu yao. |
18. | Siku hiyo Bwana atawaondolea uzuri wa njuga zao, na kaya zao; |
19. | na pete za masikio, na vikuku, na taji zao; |
20. | na dusumali, na mafurungu, na vitambi, na vibweta vya marashi, na matalasimu; |
21. | na pete, na azama, |
22. | na mavazi ya sikukuu, na debwani; na shali, na vifuko; |
23. | na vioo vidogo, na kitani nzuri, na vilemba, na utaji. |
24. | Hata itakuwa ya kuwa badala ya manukato mazuri kutakuwa uvundo, na badala ya mishipi, kamba; na badala ya nywele zilizosukwa vizuri, upaa; na badala ya kisibau, mavazi ya kigunia; na kutiwa alama mwilini kwa moto badala ya uzuri. |
25. | Watu wako waume wataanguka kwa upanga, na mashujaa wako vitani. |
26. | Na malango yake yatalia na kuomboleza, naye atakuwa ukiwa, atakaa chini. |
← Isaiah (3/66) → |