← Isaiah (29/66) → |
1. | Ole wa Arieli, Arieli, mji ambao Daudi alifanya kituo chake ndani yake; ongezeni mwaka baada ya mwaka; sikukuu na zirudi wakati wake, |
2. | ndipo nitamwudhi Arieli; kutakuwapo maombolezo na kilio; naye atakuwa kwangu kama Arieli. |
3. | Nami nitapiga kimo juu yako pande zote, nitakuhusuru kwa ngome, nami nitajenga maboma yakuzunguke. |
4. | Nawe utashushwa, nawe utanena toka chini ya nchi, na maneno yako yatakuwa chini toka mavumbini; na sauti yako itakuwa kama sauti ya mtu mwenye pepo, ikitoka katika nchi, na matamko yako yatanong'ona toka mavumbini. |
5. | Lakini wingi wa adui zako utakuwa kama mavumbi membamba, na wingi wao watishao utakuwa kama makapi yapitayo; naam, itakuwa mara na kwa ghafula. |
6. | Naye atajiliwa na Bwana wa majeshi kwa ngurumo, na tetemeko la nchi, na sauti kuu, na chamchela, na tufani, na mwali wa moto uteketezao. |
7. | Na wingi wa mataifa wapiganao na Arieli, wote wapiganao naye na ngome yake, nao wamwudhio, watakuwa kama ndoto, na maono ya usiku. |
8. | Tena itakuwa kama mtu mwenye njaa aotapo, kumbe, anakula; lakini aamkapo, nafsi yake haina kitu; na kama mtu mwenye kiu aotapo, kumbe, anakunywa; lakini aamkapo, kumbe, anazimia, na nafsi yake inatamani; hivyo ndivyo utakavyokuwa huo wingi wa mataifa waletao vita juu ya mlima Sayuni. |
9. | Ngojeni mstaajabu; fanyeni anasa zenu na kuwa vipofu; wamelewa wala si kwa mvinyo; wamewaya-waya wala si kwa sababu ya kileo. |
10. | Kwa maana Bwana amewamwagieni roho ya usingizi, amefumba macho yenu, yaani, manabii; amefunika vichwa vyenu, yaani, waonaji. |
11. | Na maono yote yamekuwa kwenu kama maneno ya chuo kilichotiwa muhuri, ambacho watu humpa mtu aliye na maarifa, wakisema, Tafadhali ukisome hiki; akasema, Siwezi, kwa kuwa kimetiwa muhuri; |
12. | kisha chuo hiki apewa mtu asiye na maarifa, akaambiwa, Kisome hicho tafadhali, akasema, Sina maarifa mimi. |
13. | Bwana akanena, Kwa kuwa watu hawa hunikaribia na kuniheshimu kwa vinywa vyao, bali mioyo yao wamefarakana nami, na kicho chao walicho nacho kwangu ni maagizo ya wanadamu waliyofundishwa; |
14. | kwa sababu hiyo mimi nitafanya tena kazi ya ajabu kati ya watu hawa, kazi ya ajabu na mwujiza; na akili za watu wao wenye akili zitapotea, na ufahamu wa wenye busara wao utafichwa. |
15. | Ole wao wanaojitahidi kumficha Bwana mashauri yao, na matendo yao yamo gizani, nao husema, Ni nani atuonaye? Nani atujuaye? |
16. | Ninyi mnapindua mambo; Je! Mfinyanzi ahesabiwe kuwa kama udongo; kitu kilichofinyangwa kimnene yeye aliyekifinyanga, Hakunifinyanga huyu; au kitu kilichoumbwa kimnene yeye aliyekiumba, Yeye hana ufahamu? |
17. | Je! Si muda mdogo uliobaki, na Lebanoni itageuzwa kuwa shamba lizaalo sana, na lile shamba lizaalo sana litahesabiwa kuwa msitu? |
18. | Na katika siku hiyo viziwi watasikia maneno ya hicho chuo, na macho ya vipofu yataona katika upofu na katika giza. |
19. | Wanyenyekevu nao wataongeza furaha yao katika Bwana, na maskini katika wanadamu watafurahi katika Mtakatifu wa Israeli. |
20. | Kwa maana mwenye kutisha ameangamizwa, naye mwenye dharau amekoma, nao wote watazamiao uovu wamekatiliwa mbali; |
21. | hao wamfanyao mtu kuwa amekosa katika neno, na kumtegea mtego yeye aonyaye langoni, na kumgeuza mwenye haki kwa kitu kisichofaa. |
22. | Basi, Bwana aliyemkomboa Ibrahimu asema hivi, katika habari za nyumba ya Yakobo; Yakobo hatatahayarika sasa, wala uso wake hautabadilika rangi yake. |
23. | Bali atakapowaona watoto wake, walio kazi ya mikono yangu, katikati yake, wao watalitakasa jina langu; naam, watamtakasa Mtakatifu wa Yakobo, nao watamcha Mungu wa Israeli. |
24. | Hao nao wakosao rohoni mwao watapata kufahamu, na hao wanung'unikao watajifunza elimu. |
← Isaiah (29/66) → |